Maabara za chanjo za BioNTech na mRNA zawasili Rwanda
14 Machi 2023Shehena ya kwanza iliyobeba vifaa vya kutengeneza chanjo kutoka kampuni ya Ujerumani ya BioNTech vimewasili nchini Rwanda jana Jumatatu, wakati bara hilo likijaribu kuimarisha uwezo wake wa kuzalisha chanjo.
Vifaa hivyo, vilivyotengenezwa kwa makontena yaliyochakatwa tena viliwasili katika mji mkuu wa Kigali, ambapo vitakusanywa ili kutengeneza kiwanda cha uzalishaji wa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Kiwanda hicho cha mjini Kigali kitakuwa na uwezo wa kuzalisha hadi chanjo milioni 100 za mRNA kwa mwaka na kitachukua angalau miezi 12 kabla ya kuanza kutoa dozi. Janga la Covid-19 lilidhihirisha utegemezi mkubwa wa afrika katika uagizaji wa chanjo kutoka nje.
Kwa mujibu wa kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa CDC, chini ya asilimia 50 ya watu bilioni 1.2 barani humo wamechanjwa kikamilifu dhidi ya Covid-19.