EU yahimiza misaada zaidi ya kijeshi kwa Ukraine
31 Januari 2024Viongozi wa nchi tano za Umoja wa Ulaya wamezihimiza nchi jirani na nchi washirika kuongeza misaada ya kijeshi kwa Ukraine, huku mawaziri wa ulinzi wa Umoja huo wakijadili njia za kuisaidia Ukraine inayokabiliwa na upungufu wa silaha.
Katika ombi lao, viongozi wa Ujerumani, Jamhuri ya Czech, Denmark, Estonia, na Uholanzi wamesisitiza kwamba usalama wa bara Ulaya unahusishwa na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametoa wito kwa nchi za Ulaya kuharakisha usafirishaji wa silaha zaidi kupelekwa nchini Ukraine, akisema kuwa hilo sio jukumu la Ujerumani peke yake.
Soma pia: Scholz atoa wito kwa wakulima kabla ya maandamano
Scholz ameongeza kusema, "ni muhimu sana kupata uungwaji mkono wa nchi za Ulaya. Tunataka nchi zaidi zishiriki kikamilifu katika kuiunga mkono Ukraine, ikiwa ni pamoja na kuipelekea silaha."
Kansela wa Ujerumani amesema nchi yake imewasilisha mifumo ya ulinzi wa anga, vifaru na silaha nyingine kwa Ukraine miongoni mwa misaada mingine mingi tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake karibu miaka miwili iliyopita.
Mahakama ya ICJ kuamua kuhusu inayoikabili Urusi
Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa (ICJ) inatarajiwa kutoa uamuzi hii leo Jumatano kuhusu madai ya Ukraine kwamba Urusi iliwafadhili waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine miaka kumi iliyopita na inaendelea kuibagua jamii ya makabila mbalimbali katika Rasi ya Crimea tangu Urusi ilipochukua eneo hilo.
Kesi hiyo, iliwasilishwa mwaka 2017, ambapo Urusi inatuhumiwa kwa kukiuka mikataba, ubaguzi na ufadhili wa ugaidi.
Ukraine inaitaka mahakama hiyo iiamuru Urusi kulipa fidia kwa mashambulizi na uhalifu katika eneo la mashariki ya Ukraine ikiwa ni pamoja na mkasa wa kuangushwa kwa ndege ya shirika la ndege la Malaysia nambari 17.
Soma pia: Biden and Scholz kujadiliana juu ya msaada mpya kwa Ukraine
Inadaiwa kuwa waasi wanaoungwa mkono na Urusi waliidungua ndege hiyo mnamo Julai 17, mwaka 2014 ambapo abiria wote 298 na wafanyakazi walikufa.
Wakati huo huo, Urusi na Ukraine zimesema leo zimekamilisha zoezi la kubadilishana wafungwa, ambalo ni la kwanza tangu ilipotokea ajali ya ndege ya jeshi la Urusi wiki iliyopita. Urusi ilisema ndege hiyo ilikuwa imewabeba wanajeshi 65 wa Ukraine.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kila upande umekabidhi kwa mwenzake askari 195 na kwamba askari wake watasafirishwa hadi mjini Moscow kwa ajili ya kupatiwa matibabu na ushauri wa kisaikolojia.
Vyanzo: AP/RTRE