Visa vya maambukizi ya corona vyaongezeka Afrika
27 Machi 2020Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mapema wiki hii alitangaza kusimamishwa kwa shughuli zote nchini humo, hatua iliyoshuhudia uchumi wa taifa hilo kubwa kiviwanda barani Afrika kwa kiasi kikubwa pia ukisimama.
Asubuhi ya leo, raia wameamka na kukutana na taarifa mbaya ya kifo kilichosababishwa na maradhi ya COVID-19, imesema wiyara ya afya kwenye taarifa yake na kuongeza kuwa visa vya maambukizi vimeongezeka na kupindukia 1,000, kutoka 927 siku ya Alhamisi.
Agizo la kusimamisha shughuli zote nchini Afrika Kusini litakalodumu kwa siku 21 limeanza kutekelezwa Alhamisi usiku na kuwataka watu kubaki ndani, na wanaweza kutoka nje kwa mambo ya lazima kama kununua vyakula ama dharura za kiafya.
Kinshasa kuanza vizuwizi Jumamosi
Huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia hatua kama hiyo inaanza kutekezwa siku ya Jumamosi na kudumu kwa siku nne katika harakati za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.
Kulingana na Gavana Gentiny Ngobila, jiji hilo litasitisha shughuli zake kwa siku hizo nne na kufuatiwa na siku mbili za kuruhusu raia kufanya manunuzi na baadaye kufuatiwa na siku nyingine nne za kusitisha tena shughuli, katika mzunguko utakoendelea kwa kipindi cha wiki tatu.
Hata hivyo, hatua hii inachukuliwa katika wakati ambapo kuna hali ngumu ya upatikanaji wa maji na watumishi wengi hawajalipwa mishahara. Tayari watu watano wamefariki kutokana na COVID-19, kati ya wagonjwa 54 walioambukizwa.
Kifo cha kwanza Kenya
Serikali ya Kenya imetangaza kifo cha kwanza kilichosababishwa na ugonjwa wa COVID-19, wakati taifa hili hapo jana likithibitisha visa 31. Mgonjwa aliyekufa ni raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 66, na alisafiri hivi karibuni akitokea Afrika Kusini.
Tayari mamlaka zimekwishatangaza zuio la watu kutembea kuanzia majira ya saa 11 za jioni hadi saa 11 alfajiri, agizo linaloanza kutekelezwa Ijumaa jioni.
Uganda nayo imeripoti visa vipya vinne, wakati jiji la Kampala likiendelea kushuhudia utulivu, baada ya vipigo vya polisi dhidi ya raia wanaokiuka maagizo ambavyo hata hivyo vimekosolewa vikali na watetezi wa haki za binaadamu na serikali yenyewe.
Burkina Faso, ambayo wiki iliyopita ilirekodi kifo cha kwanza katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara imetangaza kwamba miji minane, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Ouagadougou, huenda ikasimamisha shughuli zake kuanzia Ijumaa.