Vita na muhula mwingine wa Trump kugubika mkutano wa G20
15 Novemba 2024Kama kawaida katika mikutano ya viongozi wakuu, usalama umeimarishwa zaidi mjini Rio De Jeneiro hasa baada ya jaribio la shambulio la bomu siku ya Jumatano nje ya Mahakama ya Juu ya Brazil huko Brasilia.
Brazil inashikilia urais wa zamu wa G20 mwaka huu na imeweka kipaumbele katika kupambana na njaa, umaskini na ukosefu wa usawa.
Rais wa mrengo wa kushoto wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva atatumia fursa ya mkutano huu kuangazia nafasi yake kama kiongozi anayetetea masuala ya mataifa ya kusini lakini pia akishirikiana na nchi za Magharibi.
Jukumu ambalo litakuwa mtihani katika siku zijazo wakati Amerika ya Kusini na maeneo mengine yakitazama kwa makini sera ya "Amerika Kwanza" iliyoahidiwa na Donald Trump atakaporudi rasmi madarakani mnamo Januari.
Mkutano wa mwisho kwa Biden, Putin aupa kisogo
Katika mkutano huu rais anayemaliza muda wake Joe Biden ambaye atawakilisha taifa hilo kubwa kiuchumi duniani, kwa unyonge wakati viongozi wa mataifa mengine wakitafakari yajayo.
Mkutano wa G20 unafanyika sambamba na mkutano wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wa COP29 nchini Azerbaijan -- na wakati dunia ikipitia matukio ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na Brazil ambapo mafuriko, ukame na moto wa misitu umesababisha madhara makubwa.
Katika mkutano uliopita wa G20, nchini India, viongozi walitoa wito wa kuongezeka mara tatu kwa vyanzo vya nishati mbadala ifikapo mwisho wa muongo mmoja, lakini bila kushinikiza kwa uwazi kukomeshwa kwa matumizi ya nishati ya kisukuku.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, amekataa kuhudhuria mkutano huo akisema kuwepo kwake kunaweza "kuharibu" mkutano huo lakini atawakilishwa na Waziri wake wa mambo ya nje.
Putin amepuuza waranti ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi yake, kutokana na hatua za Urusi nchini Ukraine.
Xi wa China kuhudhuria na Afrika Kusini kupokea kijiti cha uenyekiti
Rais Xi Jinping wa China, hata hivyo, atahudhuria, na anatarajiwa kusalia kwa muda zaidi baada ya mkutano huo, kufanya ziara rasmi nchini Brasil siku ya Jumatano.
China ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Brazil, na nchi hizo mbili zimekuwa zikijitangaza kuwa wapatanishi wa kusaidia kumaliza vita vya Urusi nchini Ukraine, lakini bila mafanikio yoyote kufikia sasa.
Mikutano ya hivi majuzi G20 ilidhihirisha mfarakano kati ya nchi zinazoshiriki katika vita vya Urusi nchini Ukraine, huko Bali mnamo 2022 na Delhi mnamo 2023, na hata kutopiga picha ya pamoja ambayo kawaida viongozi husimama pamoja katika ishara ya umoja kwa sababu ya misimamo tofauti.
Xi pia alimsuta Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau katika mkutano wa Bali baada ya maelezo ya mazungumzo yao kuvuja kwa vyombo vya habari.
Mkutano wa kilele wa G20 mjini Rio utafunguliwa Jumatatu huku Lula akizindua rasmi "Muungano wa Kimataifa dhidi ya Njaa na Umaskini", Mpango ambao unalenga kuhamasisha mataifa na mashirika ya kimataifa kutoa ufadhili kwa kampeni hiyo, au kuiga programu ambazo zimefanikiwa hapo awali.
Baada ya kuwa mwenyekiti wa zamu Brazil itakabidhi urais wa G20 kwa Afrika Kusini.