Waasi Libya waendelea kumsaka Gaddafi
26 Agosti 2011Kwa upande mwengine waasi hao wameanza kuhamishia makao yao mjini Tripoli kutoka Benghazi.
Mmoja wa maafisa wa juu ya waasi, Kanali Hisham Buhagiar amesema wanayalenga maeneo kadhaa katika harakati zao za kumsaka Kanali Gaddafi, ambapo wametuma kikosi hicho maalum.Amesema wana kikosi kimoja ambacho kinafanya kazi za kijasusi na kingine kumsaka Gaddafi na wanawe.
Mapema Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Liam Fox alikiri kuwa NATO inawasaidia waasi kwa vifaa na utaalum wa kijasusi katika kumsaka Kanali Gaddafi.Aidha taarifa zinasema kuwa majasusi wa Marekani nao pia wako nchini Libya katika kazi hiyo ya kumsaka Gaddafi lakini bila ya taarifa rasmi
Nao askari watiifu kwa Kanali Gaddafi bado wameendelea kuwepo katika maeneo kadhaa mjini Tripoli ambapo mwandishi wa Reuters aliyeko mjini humo amesema baadhi ya wanajeshi hao wamekuwa wakipeperusha mabango na bendera za waasi badala ya zile za utawala wa Gaddafi.
Katika maeneo ya uwanja wa ndege waasi wanapanga kuanzisha kampeni kubwa ya kijeshi, kuwasaka askari waliyobakia wa Kanali Gaddafi.
Baada ya mapambano makali hapo jana waasi walifanikiwa kudhibiti uwanja huo wa ndege ambapo kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Al Arabiya ndege zilizokuwa katika uwanja huo ziliharibiwa kufuatia maroketi yaliyofyatuliwa na wanajeshi watiifu kwa Kanali Gaddafi.
Mapema leo mapigano yameripotiwa kutokea katika pande zote za jirani na uwanja huo wa ndege pamoja na katikati ya Tripoli.Wakaazi wa mjini hapo wamesema kuwa ndege za NATO ambazo mchango wake ulikuwa muhimu katika kuuteka mji huo zilivinjari katika anga ya mji huo usiku wa kuamkia leo.
Kumekuwa na taarifa za idadi ya watu wengi kujeruhiwa ama kuuawa ambapo hospitali zimefurika wagonjwa huku ikiarifiwa kuwepo na uhaba wa dawa.Msemaji wa utawala wa Kanali Gaddafi Mussa Ibrahim amezitupia lawama nchi za magharibi kwa mauaji yanayotokea nchini humo.
´´Kila tone la damu ya mlibya, linalomwagwa na hawa waasi , hiyo imesababishwa na ulimwengu wa magharibi, na hususan nchi wanachama wa NATO, kwa hiyo Rais Obama, Sarkozy na Waziri Mkuu Cameron kuwa wao ndiyo wenye kuwajibika zaidi na mauaji yote hayo yasiyo na ulazima ambayo yanatokea hapa nchini´´
Waasi leo wamesema kuwa wanatarajia kufanya mashambulio makubwa katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo ili kuweza kufungua barabara kuu inayoelekea Tunisia.Eneo hilo inaarifiwa kuwa limezingirwa na wanajeshi watiifu kwa Kanali Gaddafi.
Kamanda wa moja ya makundi ya waasi katika mji wa Sabratha kwenye eneo hilo, Bilal Mansur amesema hii leo wanatarajia wapiganaji zaidi kufika kwenye eneo hilo kuongeza nguvu kukabiliana na vikosi vya Gaddafi.Hata hivyo amesema idadi imepunguzwa kwani wengi wa wapiganaji wa waasi hao wamepelekwa mji mkuu Tripoli.
Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AP/ZPR
Mhariri:Josephat Charo