Waasi wa Libya waukaribia mji wa Sirte
28 Agosti 2011Kwa mujibu wa msemaji mmoja, mazungumzo yanafanywa, kumtaka Gaddafi ajisalimishe, lakini ikiwa hayatofanikiwa, basi waasi watashambulia.
Lakini, msemaji wa Baraza la Mpito la waasi, Mahmoud Shammam amesema, hakuna uhakika kuwa waasi watamkuta Gaddafi katika mji huo na wala hawajui kwa hakika, kule aliko.
Wakati huohuo, Shirika la Haki za Binadamu la Human Right Watch limesema, majeshi ya Gaddafi huenda ikawa, yaliwaua wafungwa na raia kadhaa, wakati waasi walipokuwa wakiingia mji mkuu Tripoli, wiki iliyopita.
Shirika hilo limesema, miili kadhaa iliyokuwa imepigwa risasi iligunduliwa ufukweni mwa mto karibu na eneo la makaazi ya Gaddafi.
Umoja wa Nchi za Kiarabu umetoa mwito kwa nchi wanachama wake na Umoja wa Mataifa kuachia mali ya Libya iliyozuiliwa, kwani sasa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi ameondolewa madarakani.