Wadau wahimizwa kukitumia Kiswahili katika tafiti
5 Julai 2023Mbali na kutakiwa kuitumia katika tafiti lugha ya Kiswahili wito pia umetolewa wa kukipenda Kiswahili na kukithamini sio tu kwenye mikutano ya kisiasa bali katika mazingira yote ya maisha ambayo wataalamu na watumiaji wa Kiswahili wanakutana nayo.
Wito huo umetolewa katika mjadala wa wazi ambao umewashirikisha watumiaji wa misamiati ya Kiswahili na watafiti kutoka vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi wakati wa kujadili mada isemayo Kiswahili nyenzo ya ukombizi wa fikra kwa maendeleo ya kiuchumi Barani Afrika.
Professa Amani Lusekelo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye ni mbobezi wa lugha za kigeni ameonesha namna wataalamu wanavyofanya tafiti zao kwa lugha za kigeni badala ya Kiswahili.
Pamoja na kuwataka watafiti kuweka kumbukumbu za lugha ya Kiswahili na kusisitiza wataalamu wa Tanzania kuanza kufanya tafiti zao kwa lugha ya Kiswahili ili nchi nyengine za Afrika waige mfano huo.
Wataalamu hao wametaka lugha ya Kiswahili ipewe hadhi sawa na lugha nyengine ili kuvisaidia vizazi vinavyokuja kupata kushuhudia thamani ya lugha yao ambayo ndio yenye kuwaunganisha waafrika. Professa Patrick Lumumba kutoka Kenya aliituliza hadhira uliyokuwa mbele yake ikimsikiliza kwa kutumia misemo la lafdhi iliyowavutia wengi.
Kesho kumeandaliwa matembezi rasmi ya washiriki wote wa lugha ya Kiswahili na keshokutwa kutakuwa na ufunguzi rasmi wa siku ya Kiswahili duniani ambapo kilele chake kinakhitimishwa Ijumaa hiyo ya Julai saba kwa kuhudhuriwa na viongozi wa kuu wa nchi.