Wajerumani wapiga kura kulichagua bunge
24 Septemba 2017Mpinzani wake mkubwa wa kiti cha Ukansela ni mkuu wa chama cha Social Democratic SPD, ambacho hadi uchaguzi huu kilikuwa mshirika katika serikali ya Muungano pamoja na CDU.
Wajerumani wanapiga kura leo Jumapili katika uchaguzi ambao unatarajiwa kushuhudia kansela Angela Merkel akishinda muhula wa nne wa kihistoria na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kikitarajiwa pia kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika muda wa zaidi ya nusu karne.
Kundi la kihafidhina la kansela Merkel linaelekea kubaikia kuwa kundi kubwa bungeni , uchunguzi wa maoni ya wapiga kura umeonesha kabla ya kura hiyo leo, lakini mgawanyo wa wa makundi ya kisiasa utamuwia vigumu kuunda serikali ya mseto kuliko hapo nyuma.
Wakati karibu theluthi ya Wajerumani hawajaamua wachague chama gani wakati wa kuelekea upigaji kura, Merkel na hasimu wake mkubwa katika kinyang'anyiro hiki, mgombea wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto Martin Schulz wa chama cha Social Democratic SPD, amewahimiza wapiga kura jana Jumamosi kujitokeza na kupiga kura.
"Tunataka kuwapa hamasa zaidi ili tuweze kuwafikia watu wengi zaidi ," kansela mwenye umri wa miaka 63, alisema mjini Berlin kabla ya kuelekea kaskazini katika jimbo lake kwa ajili ya duru ya mwisho ya kampeni.
Uchaguzi wa majimbo pigo kwa Merkel
Katika uchaguzi wa majimbo mwaka jana, chama cha kansela Merkel cha kihafidhina kilipata pigo dhidi ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD , chama mbadala kwa Ujerumani, ambacho kilifaidika na hali ya wapiga kura kutoridhishwa na uamuzi wake kuweka mipaka ya Ujerumani wazi kwa ajili ya wahamiaji milioni moja.
Hali hiyo ya kushindwa ilimfanya Merkel , ambae ni binti wa mchungaji ambaye alikulia katika Ujerumani ya mashariki ya kikomunist, kufikiria iwapo ajaribu kugombea kuchaguliwa tena.
Lakini baada ya suala hilo la wakimbizi kulidhibiti mwaka huu, alirejea tena katika umaarufu na kujitupa tena kufanya kampeni , akijiwakilisha kuwa ni mhimili wa uthabiti katika dunia ambayo haina uhakika.
Chama cha siasa kali za mengo wa kulia
Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Alexander Gauland, muasisi mwenza na naibu mwenyekiti wa chama hicho cha AfD amesema "tutairejesha nchi yetu kwenu kwa kuzuwia mmiminiko wa wakimbizi." Katika suala la kuunda serikali ya mseto ambapo vyama vya muda mrefu SPD, na CDU vimesema havitafikiria kuungana na chama hicho kuunda serikali, kiongozi wa chama cha AfD Gauland amesema "hatutaingia katika muungano na chochote kati ya vyama hivyo pia. Tutabakia kuwa chama cha upinzani tukiwa na msimamo thabiti."
Uchaguzi wa leo wa taifa nchini Ujerumani utaashiria mwanzo wa mjadala mpya hata hivyo katika kuweka sawa mapungufu kuhusiana na sarafu ya pamoja ya euro.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameweka wazi kwamba anapendelea kusukuma mageuzi ili kuimarisha sarafu ya euro na anatarajiwa kutoa mapendekezo katika hotuba yake muhimu siku ya Jumanne.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape