Wajerumani wenye asili ya Afrika walenga kuvunja vikwazo
17 Agosti 2023Watu wenye asili ya Kiafrika wanafanya kazi katika taaluma nyingi nchini Ujerumani: Wanaweza kuwa wanafanya kazi kama wauza maduka, wafanyakazi wa huduma, wanamuziki na watoa huduma. Pia wanazidi kuwakilishwa katika vyombo vya habari, katika vyuo vikuu na maeneo mengine ya maisha ya umma.
Lakini kwa miaka kadhaa sasa, wameanza pia kuchukua nafasi kuu katika siasa.
"Uwepo wa watu Weusi unaonekana hasa katika siasa. Wanasimamia jamii ambayo ni tofauti zaidi kuliko inavyodhaniwa mara nyingi," alisema Tahir Della, msemaji wa Jumuiya ya Watu Weusi nchini Ujerumani, ISD.
Katika mahojiano, aliiambia DW kuwa inafurahisha kuona watu waliokulia Ujerumani na ambao ni sehemu ya miundo yote iliyopo pia wanawakilishwa kwa njia hii.
Jumuiya hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1985, inakadiria idadi ya watu wenye asili ya Kiafrika nchini Ujerumani kufikia karibu milioni 1.2. Ingawa idadi hii inaweza kuonekana kuwa ya chini kwa mtazamo wa kwanza, Della anasema pia inamaanisha kuwa hawajawakilishwa sawia katika jamii.
Joe Chialo: Seneta mgumu wa utamaduni
Joe Chialo ni miongoni mwa Wajerumani Weusi wanaojijengea jina kufuatia kuchaguliwa kwake kama seneta wa utamaduni wa Berlin mnamo Aprili 27.
Anajua athari za kiuchumi za tasnia hii kwa Berlin, na pia anafahamu wajibu unaokuja nayo. "Ninafahamu kikamilifu kwamba seneta anayemaliza muda wake wa masuala ya utamaduni [Volker Lederer - notisi ya Mhariri] ni maarufu sana hapa jijini, na kwamba miaka ijayo itakuwa na changamoto nyingi," Chialo aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa.
Chialo alizaliwa Bonn mwaka 1970 katika familia ya wanadiplomasia wa Tanzania. Baadaye alihudhuria shule ya bweni ya Kikatoliki karibu na Cologne pamoja na kaka yake.
Soma pia:Neno "Nafri" laiweka pabaya polisi ya Ujerumani
Hata hivyo, taaluma ya kisiasa ya Chialo mwenye umri wa miaka 52 imejumuisha vituo visivyo vya kawaida njiani. Chialo alifunzwa kama mkataji wa viwanda katika kinu cha usindikaji, alisoma historia, siasa na uchumi kwa mihula michache kisha akaacha kufuata mapenzi yake ya muziki.
Alijiunga na bendi ya Hard Rock ya Blue Manner Haze, ambayo ilikuwa na mafanikio kadhaa katika miaka ya 1990. Karibu wakati huo huo, alijiunga na chama cha siasa cha watetezi wa mazingira, die Grüne.
Miaka kadhaa baadaye, alihama na kujiunga na chama cha mrengo wa kulia cha Christian Democratic Union (CDU) mwaka 2016 - lakini tu kutokana na kuunga mkono sera ya wakimbizi ya Kansela wa zamani Angela Merkel.
Chialo alijulikana kote nchini alipoteuliwa kuwa kwenye "timu ya siku zijazo" ya mgombea ukansela wa wakati huo Armin Laschet, wakati wa uchaguzi wa shirikisho wa 2021. Laschet alishindwa uchaguzi, na Chialo alipoteza nafasi yake ya kuwa na ofisi katika Bundestag, bunge la kuchaguliwa la Ujerumani.
Hata hivyo, katika mpango mkubwa zaidi wa mambo, hii ilikuwa ni kikwazo kidogo tu kwa Chialo, ambaye anajieleza kama "Afropean," yaani Muulaya Mwafrika.
Kwa kweli, mitazamo yake mpya juu ya maswala mengi makuu ya kisasa imemsaidia kupata ufuasi mkubwa. Kuanzia kupinga maoni ya Ulaya kuhusu Afrika hadi kushughulikia jinsi Kanisa Katoliki linavyoshughulikia kesi za unyanyasaji na kushindwa kwa Ujerumani kudhibiti mabadiliko yake ya kidijitali, Chialo amevutia watu wengi na anatazamwa kushoto, kulia na katikati kwa malengo yake ya baadaye ya kisiasa.
Soma pia:Obama na waafrika Ujerumani
Della alisema Chialo anathaminiwa sana kwa maoni yake ya kipekee, lakini anasisitiza kuwa, iwapo anaweza kuimarisha mustakabali kama nguvu thabiti ya mabadiliko hilo bado halijulkani.
"Kwa maoni yangu, ni kwa sifa ya vuguvugu la vijana Weusi kwamba watu Weusi sasa wanazidi kushiriki katika mchakato wa kisiasa, kuchangia misimamo yao na hivyo pia kuchangia katika jamii ambayo ina sifa ya utofauti na haki," Della aliiambia. DW.
Aminata Toure: Waziri wa kwanza wa serikali mwanamke Mweusi
Aminata Toure pia anapiga hatua katika madaraja ya kisiasa ya Ujerumani. Yeye ni mwanamke wa kwanza, waziri wa serikali Mweusi katika jimbo lake la nyumbani la Schleswig-Holstein, akiongoza Wizara ya Masuala ya Kijamii, Vijana, Familia, Wazee, Ushirikiano na Usawa tangu katikati ya 2022.
Toure alizaliwa Neumünster mnamo 1992, ambapo alikulia katika makazi ya wakimbizi. Wazazi wake walikuwa wameihama nchi yao ya Mali baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1991. Toure hakupewa hata uraia wa Ujerumani hadi alipokuwa na umri wa miaka 13.
Toure aliendelea kusoma sayansi ya siasa na fasihi ya Kifaransa, baadaye akajihusisha na Chama cha Kijani.
Mnamo 2017, alijiunga na bunge la jimbo la Schleswig-Holstein mjini Kiel, na kuwa naibu spika miaka miwili tu baadaye - mtu mdogo zaidi kuwahi kushika wadhifa huu na Mwafrika Mjerumani wa kwanza. Na amepamba vichwa vya jarida la Vogue la Ujerumani.
Katika mahojiano na jarida hilo la mitindo, Toure alionekana kujiamini, akionyesha umuhimu wa kupambana na ubaguzi wa rangi na kuunga mkono ujumuishwaji wa wakimbizi.
Soma pia: Mwanasiasa mwenye asili ya Afrika aapishwa kama waziri nchini Ujerumani
Aliliambia jarida hilo la mitindo na mtindo wa maisha kuwa michakato ya kisiasa inahitaji kuwa wazi zaidi ili kufikia makundi ya kijamii ambayo hayajali siasa.
Della alisema hadithi ya Toure inaangazia jinsi watu wa rangi zote wanavoweza kufikia mafanikio na kuwa na sifa bora zaidi nchini Ujerumani. "Huwezi kukataa kwamba kuna kitu kimebadilika katika miaka 10 hadi 20 iliyopita" kuhusiana na mitazamo ya ubaguzi wa rangi nchini Ujerumani, alisema.
Steffi Jones: Mfano wa kuigwa ndani na nje ya uwanja
Stephanie Ann Jones, anayejulikana kama "Steffi," ni mmoja wa wachezaji wa soka wa Ujerumani waliofanikiwa zaidi.
Bingwa huyo wa dunia wa 2003 na bingwa mara tatu wa Ulaya alistaafu mnamo 2007, hatua iliyofuatiwa na kuteuliwa kwake kuwa rais wa Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia la Wanawake la 2011.
Binti huyo wa mwanajeshi Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika na mama Mjerumani aliendelea kuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Ujerumani - wadhifa alioshikilia kuanzia 2016 hadi 2018.
Soma pia: Neid kujiuzulu kama kocha wa timu ya wanawake ya Ujerumani
Na kisha akaamua kusema kwaheri kwa mchezo huo mzuri, na kuanza kazi mpya kama mjasiriamali katika tasnia ya programu za computer.
Hata hivyo, licha ya mafanikio yake ya kushangaza, Jones, pia, amekumbana na ubaguzi wa kawaida wa rangi. Amelazimika kukabiliana na matusi anayotupiwa kwenye uwanja wa soka.
Della alisema hata hivyo, mambo yamekuwa rahisi kwa watu wa rangi mbalimbali pia katika michezo, ambapo wanaweza kuleta mabadiliko na kuacha urathi wa kudumu unaopiku mafanikio yao uwanjani.