Waliouawa kwenye maandamano DRC kuzikwa Ijumaa
5 Agosti 2022Waandamani wa Goma wanashiriki mazishi ya watu 10 waliokufa katika machafuko hayo, baada ya serikali pamoja na familia zao kukubaliana kuhusu mazishi hayo.
Ili kufanikisha mazishi ya wahanga wa mauwaji yaliyofuatia maandamano ya kuipinga MONUSCO, serikali ya Kongo ilikabidhi kwa kila familia dola za Kimarekani elfu mbili, kwa mjibu wa duru za karibu na gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini.
Kitita hicho cha pesa kinaonekana kuwa hakitoshi kukidhi mahitaji ya wajane pamoja na yatima, kama anavyoueleza Mumbere Jacques, mmoja wa wawakilishi wa familia za wahanga wa mauwaji yaliyotokana na maandamano ya mjini Goma yaliyofanyika kwa siku 12 zilizopita.
Watu wasiopungua 30 waliuawa na zaidi ya 100 walijeruhiwa, katika mfululizo wa maandamano hayo katika miji ya Goma, Kanyabayonga, Butembo na Kasindi.
Tangazo la serikali ya Kongo kutaka kuondoka haraka kwa Mathias Gillman, msemaji wa MONUSCO nchini humo, kunaonekana kwamba hakujawaridhisha waandamanaji, wanaoitaka tume nzima ya Umoja wa Mataifa kuondoka kama alivyoainisha Clovis Mitsuva, mwanachama wa vuguvugu la vijana kwa ajili ya mabadiliko, LUCHA.
Mazungumzo yanayopangwa kufanyika kati ya wajumbe wa serikali ya Kongo na wale wa MONUSCO ili kutathmini mpango wa kuondoka nchini humo kwa ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa hatua kwa hatua, huenda ndio utatupatia mwangaza kuhusu hatma ya tume hiyo ambayo inaonekana kutopendwa tena na baadhi ya raia wa Kongo wanaoishuku kutotekeleza vizuri majukumu yake nchini Kongo.